Manispaa ya mjini Unguja sasa kuwa jiji

Thursday May 16 2019

By Haji Mtumwa, Mwananchi [email protected]

Unguja. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi na Idara Maalumu), Haji Omar Kheir, amesema kuanzia Julai mosi 2019 Manispaa ya Mjini Unguja itapandishwa hadhi kuwa jiji.

Waziri Kheri alibainisha hayo leo Alhamisi Mei 16, 2019 katika Baraza la Wawakilishi akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Amesema uamuzi huo wa kuifanya Manispaa ya Mjini kuwa jiji unakuja baada ya kuridhiwa na Serikali katika tangazo la namba 120 la 2015.

Amesema hatua zilizochukuliwa ni kukamilisha maandalizi ya uchaguzi wa meya, naibu wake na uteuzi wa mkurugenzi wa jiji atakayeteuliwa na Rais.

Waziri amesema fedha kwa ajili ya uendeshaji wa jiji hilo zitatolewa kuanzia Julai 2019.

Akizungumzia bajeti hiyo, Kheri amesema Serikali ina mpango wa kufanya utafiti wa kubuni uwezo wa vyanzo vya mapato na udhibiti wake katika serikali za mitaa kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Amesema kufanya hivyo ni kutafuta fursa za upatikanaji wa rasilimali fedha kufanikisha utekelezaji wa programu za miradi ya maendeleo.

Katika kuimarisha ukusanyaji mapato katika serikali za mitaa, amesema ofisi yake kwa kutumia wataalamu wa ndani itaendelea kusimamia na kuhakikisha kila manispaa, baraza la mji na halmashauri inakusanya mapato kutoka katika vyanzo vyake vya mapato kwa mfumo wa kielektroniki.

Alisema hadi Machi 2019, halmashauri zote zimeunganishwa katika mfumo wa pamoja wa ukusanyaji mapato na kuanza kutumia mashine za kukusanya mapato maeneo ya maegesho, masoko na vituo vya ukusanyaji ada zitokanazo na usafirishaji wa maliasili zisizorejesheka.

Kheria amesema ofisi ina uwezo wa kuona na kufuatilia taarifa za ukusanyaji mapato kutoka kila halmashauri na kushauri ipasavyo.

Pia, amesema kwa mwaka wa fedha 2018/19 mamlaka ya serikali za mitaa zilikadiriwa kukusanya Sh12.66 bilioni hadi sasa zimekusanya Sh9.1 bilioni sawa na asilimia 72 ya makadirio.

Advertisement