Maombi ya Tundu Lissu Mahakama Kuu yakwamisha kesi ya vigogo Chadema

Muktasari:

Kesi inayowakabili vigogo wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema imeshindwa kuendelea leo Alhamisi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutokana na mawakili wanaowatetea washtakiwa hao kuwa katika kesi nyingine iliyofunguliwa na Tundu Lissu Mahakama Kuu ya Tanzania.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar  es Salaam imepanga Agosti 19, 2019, kutoa uamuzi wa kuonyesha video iliyopokelewa mahakamani kama ushahidi katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Uamuzi huo ulipaswa kutolewa leo Alhamisi Agosti 15,2019 lakini umeshindikana  kutokana na mawakili wa upande wa utetezi kuwa katika kesi nyingine Mahakama Kuu ya Tanzania.

Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, amesema atatoa uamuzi huo Agosti 19, 2019, hivyo washtakiwa wote wanatakiwa kuwepo mahakamani hapo.

"Kwa kuwa mawakili wa upande wa utetezi wapo Mahakama Kuu ya Tanzania, kesi hii naiahirisha hadi Agosti 19, 2019 nitakapotoa uamuzi " amesema Hakimu Simba.

Kabla ya Hakimu Simba, kuahirisha  kesi hiyo, wakili wa utetezi, Gaston Shundo, ameieleza  Mahakama hiyo kuwa wakili wa washtakiwa, Peter Kibatala na wenzake wapo Mahakama Kuu katika kesi ya madai namba 18/2019 iliyofunguliwa na Tundu Lissu.

Shundo amedai, Lissu amefungua maombi Mahakamani Kuu, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, akipinga kuvuliwa ubunge.

 

Amedai kuwa kesi hiyo ya maombi ya madai, ipo mbele ya Jaji Sirillius Matyupa.

Amedai katika kesi hiyo, Lissu anaomba  kupata amri  kuhusiana na uamuzi wa kuvuliwa ubunge wake.

"Hivyo kutokana na mawakili wa washtakiwa kutokuwepo mahakamani hapo, naomba mahakama yako iahirishe kesi hii," amedai Shundo.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo ya upande wa mashtaka, ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 19, 2019, atakapotoa uamuzi na kuwataka washtakiwa wote kuwepo mahakamani hapo.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai  kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya mahakama kutoa uamuzi na wako tayari kusikiliza uamuzi huo.

Itakumbukwa , Julai 26, 2019, upande wa utetezi ulipinga kuonyesha kwa mkanda wa video uliotolewa na upande wa mashtaka mahakamani.

Wakili wa washtakiwa hao, Peter Kibatala amedai upande wa mashitaka ulipaswa kuandika barua kwa uongozi wa mahakama kuomba kutumika kwa kituo cha mafunzo kuonesha maudhui  yaliyopo katika mkanda huo wa video.

Kibatala alidai  upande wa mashtaka walipaswa kuandaa vifaa vyote muhimu ikiwemo waya na projekta ambavyo vingewezesha kuonekana kwa video hiyo na sio wajibu wa mahakama kuandaa.

"Kama upande wa mashtaka wanataka kuoneshwa kwa video hiyo walipaswa kuleta mahakamani waya, projekta na vifaa vingine na kuvitoa kama kielelezo na ndipo ushahidi huo ungeweza kuoneshwa bila kupingwa" amedai Kibatala

"Kitendo cha kutumia vifaa kutoka nje ya ushahidi ulioletwa mahakamani hapo hauruhusiwi kisheria na kwamba kama kamera iliyopokelewa mahakamani ina uwezo ioneshwe kwani ushahidi utatoka hapohapo kwenye kamera na sio kufungwa kwa projekta au runinga ndani ya mahakama hii," alidai Kibatala.

Kwa upande wake Profesa Abdallah Safari ambaye naye anawatetea washtakiwa hao, alidai kuwa hata waya wa kuchajishia kamera pamoja na waya wa kuunganishia kamera na projekta au luninga, vilipaswa kutolewa kama sehemu ya vielelezo, ili baadaye vije vitumike katika kuunganisha kamera na projekta, lakini upande wa mashtaka hawa kufanya hivyo.

 

Akijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alidai mapingamizi hayo hayana msingi wa kisheria isipokuwa ni maoni binafsi.

 

"Sio kila kinacholetwa mahakamani kinapaswa kutolewa kama ushahidi na kwamba kutumia kamera na tepu ni kwa sababu ni vielelezo hivi tayari vimepokelewa na mahakama hii," alidai Kadushi.

 

Mbali na Mbowe washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu Chadema  Dk Vicent Mashinji, John Mnyika Naibu Katibu Mkuu (Chadema)-Bara na Salumu Mwalimu Naibu Katibu Mkuu Chadema Zanzibar.

 

Wengine ni wabunge, Ester Matiko (Tarime Mjini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), na Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, yakiwemo ya uchochezi, wanayodaiwa kutenda Februari 16, 2018, wakati wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Kinondoni.