Mapato ya mauzo ya korosho nje ya nchi yashuka

Muktasari:

Ripoti ya mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Desemba 2018 imeonyesha jinsi zuio la Serikali ya Tanzania la kutokuuza korosho nje ya nchi ambayo haijabanguliwa ilivyoshusha mapato ya zao hilo


Dar es Salaam. Katazo la Serikali la kuuza korosho nje ya nchi limesababisha pengo kwa Tanzania katika salio la malipo na kuwepo upungufu wa takribani Dola500 milioni kwa mwaka ulioishia Novemba 2018.

Ripoti ya mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Desemba 2018 imeonyesha mlinganyo wa jumla wa malipo wa (BoPs) ukiwa na upungufu wa Dola 753.0 milioni kwa mwaka ulioishia Novemba 2018 ikilinganishwa na upungufu wa Dola 171.6 milioni iliyorekodiwa Oktoba ya mwaka huo.

Ripoti hiyo inasema mapato ya mauzo ya korosho ambalo ni zao linaloongoza kwa mauzo ya nje ya nchi yameshuka kutokana na uamuzi wa Serikali kununua korosho za wakulima na kuzibangulia katika viwanda vya ndani.

Mauzo ya korosho nje ya nchi yamekuwa yakifikia Dola 575 milioni, mauzo hayo ambayo ni sawa na mauzo ya mazao mengine matano ya biashara kama tumbaku, chai, kahawa na katani.

Hivi karibuni Serikali ilitangaza kununua zaidi ya tani 200,000 za korosho kutoka kwa wakulima katika mikoa inayozalisha kwa wingi zao hilo tayari kwa kuuza nje ya nchi baada ya kuzibangua kwa viwanda vya ndani.