Mapingamizi yatawala kesi ya dhahabu

Sunday May 26 2019

 

By Jesse Mikofu, Mwananchi

Mwanza. Mapingamizi yameendelea kutawala kesi ya kusafirisha shehena ya kilo 319 za dhahabu yenye thamani ya Sh27.8 bilioni.

Juzi katika mahakama ya hakimu mkazi Mkoa wa Mwanza mbele ya hakimu Mkazi Mfawidhi, Rhoda Ngimilanga, wakili wa utetezi Fidelis Mtewele aliweka pingamizi lingine kwa shahidi wa nane ambaye ni meneja wa Benki ya CRDB, tawi la Nyerere Mwanza, Eugenus Shang’a asiwasilishe nyaraka za miamala ya fedha mahakamani hapo.

Hii ni baada ya shahidi wa saba, mkaguzi msaidizi wa Polisi Anderson Nyonyi pia kuwekewa pingamizi asitoe kitabu cha ukaguzi vituo vya polisi mahakamani kama kielezo, ambacho hata hivyo, mahakama ililitupa na kitabu hicho kupokewa.

Nyaraka hizo zilizowekewa pingamizi, mbili zilikuwa zinaonyesha hundi ya kutoa fedha Sh200 milioni na Sh300 milioni iliyofanyika Januari 5 mwaka huu, ya mteja wake aliyemtaja kwa jina la Michael Shegembe (shahidi wa pili katika kesi hiyo).

Pia, alidai nyaraka nyingine iliyotolewa siyo sahihi kwa sababu ilikuwa cheti cha utambulisho kutoka ofisi ya Takukuru makao makuu ikielekeza kwenda kwa ofisa wa Takuku Mkoa wa Mwanza, lakini sio barua inayoelekeza kwenda kufanya uchunguzi katika benki hiyo ambako pia utambulisho huo unaonyesha kwenda CRDB Mwanza badala ya kuelekeza tawi husika linalotakiwa kufanyiwa uchunguzi.

Pia, alidai meneja huyo si mtu sahihi kutoa nyaraka hiyo kwasababu yeye sio aliyemhudumia mteja huyo tarehe iliyotajwa, bali alihudumiwa na mfanyakazi wa benki hiyo aitwaye Lucky Matola.

Advertisement

Baada ya hoja hizo, wakili wa Serikali mkuu, Frederick Manyanda alidai kwamba kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki namba 13 ya mwaka 2015, iliyofanyiwa marekebisho kifungu cha 64 A na kifungu cha 18 cha sheria hiyo, vinaruhusu nyaraka za elektroniki kupokewa mahakamani.

Kuhusu uhalali wa meneja huyo kuwasilisha nyaraka hizo, alisema ndiye mtu sahihi kwa sababu ndiye mwenye mamlaka hayo kisheria na masuala yote ya kiutendaji yapo chini yake katika tawi hilo.

Alidai kwamba nyaraka hizo ni sahihi kupokewa na mawakili hao wangesubiri ili baadaye wamhoji.

Baada ya mabishano hayo ya kisheria, Hakimu Ngimilanga alisema ataandika uamuzi wa hoja hizo zilizowasilishwa hivyo kuahirisha shauri hilo hadi Juni 6 atakapotoa uamuzi.

Awali wakati akitoa ushahidi wake, meneja huyo alisema iwapo taarifa zote za mteja zinahitajika kutolewa kwa sababu maalumu za kiuchunguzi, lazima apokee barua kutoka Takukuru kisha yeye amjulishe mkurugenzi mkuu wa benki hiyo, aridhie na kumuandikia barua ya kumruhusu kutoa taarifa za mteja.

Washtakiwa katika shauri hilo ni pamoja na aliyekuwa mkuu wa operesheni Mkoa wa Mwanza, Morice Okinda, E 6948 D/CPL Kasala, F 1331 PL Matete, G 6885 D/C Alex na G 5080 D/C Maingu.

Wengine ni G 7244 D/C Timothy, G 1876 D/C Japhet, H 4060 D/C David Kadama ambao walifikishwa mahakamni hapo kwa mara ya kwanza Januari 11.

Advertisement