VIDEO: Mwanafunzi aliyejipiga risasi alivyomaliza siku yake ya mwisho duniani

Morogoro. Imelda Mlanzi, rafiki wa Jasmine Ngole aliyejiua kwa kujipiga risasi kooni na kufumua sehemu ya utosi, ameeleza jinsi rafiki yake huyo alivyomuachia shajara (diary) iliyokuwa na ujumbe pamoja na Sh20,000.

Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwao eneo la Bigwa mjini Morogoro, Imelda anayesoma Shule ya Sekondari Lupanga alisema aliachiwa shajara hiyo saa chache kabla ya Jasmin kukutwa amekufa.

“Aliniambia katika hizi Sh20,000, nichukue Sh10,000 na Sh10,000 nyingine nikamlipie madeni kwa watu waliokuwa wakimdai,” alisema Imelda.

Katika shajara hiyo, Jasmin aliandika,“Ni mtoto asiyewajua wazazi wake na asiyejua kazaliwa wapi? Mtoto huyu anatamani kukiona kifo chake wakati wowote, mtu yeyote atakayesoma dayari hii ndiye atakayeandika siku ya kifo chake.”

Mwili wa Jasmini ulikutwa kando ya barabara nyembamba, eneo la Kola B Manispaa ya Morogoro, alfajiri ya Jumanne iliyopita huku bastola aliyotumia kujiua, mali ya Profesa Hamis Maige iliyokuwa na magazine moja pamoja na ganda la risasi vikiwa kando yake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alisema muda mfupi baada ya tukio hilo kuwa, Profesa Maige alijitokeza na kueleza kuwa bastola hiyo ni yake na anaimiliki kihalali.

Imelda alisema Jumatatu iliyopita saa mbili usiku Jasmin alikwenda nyumbani kwao ambako mbali na kumkabidhi fedha, alimpatia kitabu cha shule pamoja na kadi ya Valentine (Siku ya wapendanao).

“Sikuweza kuifungua ile diary kwa muda ule na sikuwa na mashaka yoyote kwa kuwa Jasmin alikuwa na kawaida ya kunizawadia vitu mbalimbali. Ilipofika saa tatu usiku aliniaga akisema anarudi nyumbani kwao, nilimsindikiza na kuachana naye nje,” alisema Imelda.

Alisema siku iliyofuata akiwa darasani aliona polisi na baada ya muda walimuita wakiwa na kumuuliza kama anafahamu chochote kuhusu kifo cha Jasmin.

“Hapo ndipo nilipojua kuwa amejiua kwa kujipiga risasi. Baada ya kunihoji niliwapa diary na ndio nikagundua kuwa imeandikwa ujumbe,” alisema.

“Polisi walinichukua na kunipeleka kituo cha polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi na baada ya masaa mawili waliniruhusu kurejea nyumbani.”

Aliongeza, “Ule ujumbe aliandika Jasmin mwenyewe na niliutambua mwandiko wake kwa sababu mara nyingi huwa tunaandikiana kazi za darasani.”

Imelda ambaye muda wote wa mazungumzo alikuwa mtulivu alisema Jasmin alikuwa na tabia ya kuzungumzia kifo chake.

“Mara nyingi alikuwa akisema kifo chake kimekaribia na kwamba kitakuwa kibaya kiasi cha watu kushindwa kuuaga mwili wake,” alisema.

“Hakuwahi kueleza hali ya maisha anayoishi nyumbani kwao na hata nilipokuwa nakwenda kwao nilikuta akiishi katika maisha mazuri na hata mahitaji ya shule alikuwa akiyapata kama kawaida. Yeye na mdogo wake walikuwa wakipelekwa shule kwa gari ndogo ya nyumbani.”

Siku moja kabla ya kifo

Akizungumzia matukio aliyoyafanya Jasmin shuleni siku moja kabla ya kujiua, Imelda alisema kuwa alifika shule akiwa na Sh10,000 na kumwambia yeye na wanafunzi wenzake wale wanachokitaka na alilipa vitu vyote walivyokula huku akiwa yu mwenye furaha.

Kuhusu maendeleo yake ya kitaaluma, Imelda alisema rafiki yake huyo alikuwa na maendeleo ya wastani na alikuwa na mahudhurio mazuri na mwepesi wa kushiriki kwenye kazi na michezo.

Alisema siku moja Jasmin aliwahi kumueleza kuwa ni yatima na analelewa na Profesa Maige ambaye anamuita shemeji.

“Ila hakuwahi kunieleza kama Profesa huyo anamiliki silaha ama yeye mwenyewe (Jasmin) anaweza kutumia silaha,” alisema.

Imelda alisema kifo cha rafiki yake kimemuumiza kwa kuwa alikuwa mtu wake wa karibu na walikuwa wakishirikiana katika masomo.

Alitoa wito kwa wasichana kuwa wazi na kueleza matatizo yanayowakabili badala ya kujiua kwa kuwa kitendo hicho kinakatisha ndoto zao.

Ashindwa kufanya mtihani

Jana, Imelda alishindwa kufanya mtihani wa mwezi baada ya kuishiwa nguvu na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Akizungumza na Mwananchi, makamu mkuu wa shule hiyo, Daud Masunga alisema Imelda alifika shuleni hapo akiwa amechelewa na baadaye hali yake ilibadilika.

Alisema alikuwa mnyonge na alikuwa akilia wakati wote hali iliyosababisha walimu wamruhusu kurudi nyumbani.

“Kwa kweli Imelda bado hayuko sawa, tumejaribu kumpa ushauri nasaha lakini bado yuko kwenye taharuki ameshindwa kufanya mitihani ya mwezi na tumemruhusu arudi nyumbani,” alisema Masunga.