Mara watenga ekari 20 kuanzisha shamba darasa

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima

Muktasari:

Mkoa wa Mara umetenga eneo la ekari 20 kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa ili wananchi wapate sehemu ya kujifunza kilimo cha kisasa

Musoma. Mkoa wa Mara umetenga eneo la ekari 20 kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa ili wananchi wapate sehemu ya kujifunza kilimo cha kisasa.

Katika eneo hilo kila halmashauri mkoani Mara  itakuwa na eneo lake kwa ajili ya kuanzisha mashamba darasa ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Agosti Mosi, 2019, mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima amesema wameamua kuanzisha shamba hilo kutoa elimu  ya kilimo kwa wakazi wa Mkoa huo katika kipindi cha mwaka mzima badala ya kusubiri maonyesho ya wakulima.

“Kama unavyojua mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga kwa mwaka wa pili sasa tumepewa heshima ya kuandaa maonyesho ya nanenane kitaifa, tumeona hii haitoshi ni vyema tukasogeza huduma karibu zaidi ili wananchi wetu wapate fursa ya kujifunza kwa  ukaribu na kutekeleza kwa vitendo,” amesema Malima.

Amesema mbali na kutumika kama shamba darasa, eneo hilo litatumika katika maonyesho ya kilimo, kuuzia  mazao yatakayozalishwa katika maonyesho.

Wakizungumzia uamuzi huo baadhi ya wakazi wa manispaa ya Musoma mbali na kupongeza wameshauri  mashamba hayo kufunguliwa kwenye kila halmashauri badala ya eneo moja.

“Badala ya Mkoa mzima kutegemea shamba moja ni vyema kila Wilaya au halmashauri zikawezeshwa ili wananchi waweze kupata kilichodhamiriwa na Serikali kwa ukaribu zaidi, mashamba yafunguliwe vijijini kwa wakulima badala ya mijini,” amesema Wilson Magesa.