Marekani watoa tahadhari la shambulio la kigaidi Uganda

Muktasari:

Tahadhari hiyo imekuja siku moja baada ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania kuwatahadharisha wananchi kuhusiana na kuwapo na taarifa za sambulio la kigaidi


Kampala, Uganda. Ubalozi wa Marekani nchini Uganda umetoa tahadhari ya kuwapo kwa taarifa za shambulizo la kigaidi nchini humo.

Kwa mujibu wa tahadhari hiyo iliyochapishwa katika ukurasa wa mtandao wa kijamii wa ubalozi huo, kuna uvumi wa mipango ya mashambulizi katika maeneo yanayopendwa na raia wa kigeni katika Afrika Mashariki ikiwamo Uganda.

Shirika la habari la BBC liliunukuu ubalozi huo ukisema kuwa japokuwa hauna ushahidi wa kutosha kuhusu tishio hilo au habari kuhusu wakati ambao mashambulizi hayo yatafanyika wakazi wanapaswa kuchukua tahadhari.

"Ubalozi hauna ushahidi wa moja kwa moja wa tishio hilo au taarifa za muda gani mashambulizi yatatokea, hata hivyo unawaonya wananchi kuchukua tahadhari.

“Jeshi la polisi lilipata fununu za tishio la ugaidi kabla ubalozi wa Marekani,” ilisisitiza taarifa hiyo ya Marekani.

Tahadhari hiyo inajiri siku moja tu baada ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Tanzania kutoa tahadhari nakuwataka wakazi  kuchukua tahadhari hususan waliopo katika eneo la Masaki.

Eneo hilo lililopo kwenye rasi ya Msasani ni moja ya maeneo ya makazi ya kigahari zaidi jijini humo

Tahadhari hiyo ilibainisha kuwa, maeneo yanayolengwa ni mahoteli na migahawa ambayo hutembelewa na watalii ikiwemo eneo maarufu la maduka ya Slipway.

Tutaendelea kukujuza zaidi kadri tutakavyokuwa tunapokea taarifa juu ya tahadhari hiyo.