MUUNGANO TANGANYIKA - ZANZIBAR 1964: Marekani yaanza kukwama mpango wa Muungano - 6

Muktasari:

  • Jana tuliona jinsi Marekani ilivyokuwa ikihaha kutaka Zanzibar iingizwe katika muungano wa nchi za Afrika Mashariki, huku jitihada hizo zikitegemea ushawishi wa Mwalimu Julius Nyerere, ambaye hata hivyo ilikuwa shida kuongea naye na hivyo Marekani kuongeza nguvu kwa kumhamisha balozi wake kutoka Zaire (sasa Congo) kwenda kuwa ofisa ubalozi visiwani Zanzibar.

Marekani iliendelea kuwa na hofu kwamba Zanzibar inaweza kuwa Cuba ya Afrika iwapo wakomunisti wangefanikiwa kuwashawishi viongozi wa mapinduzi na hivyo ofisi ya mambo ya nje kuwasiliana mara kwa mara na balozi zake za Tanganyika, Uganda, Kenya na Zanzibar ama kusisitiza kuhusu mpango wa kuiingiza katika Umoja wa Afrika Mashariki au kupata taarifa ya kinachoendelea na kushauri.

Jumamosi ya Aprili 14, 1964, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, David Dean Rusk alituma ujumbe kwa balozi wake aliyekuwa Tanganyika.

Ujumbe huo ulisisitizia wazo la awali la kuwatumia Rais Jomo Kenyatta wa Kenya na Milton Obote wa Uganda na kwamba Marekani iepuke kuwasiliana moja kwa moja na Julius Nyerere kuhusu suala la Zanzibar.

Walijaribu kumtumia Kenyatta kama chombo chao cha kuwasiliana na Nyerere kumweleza kile walichotaka.“Idara (pengine akimaanisha CIA) ingetaka kupata maoni ya Balozi Leonhart ikiwa (Oscar) Kambona anaweza kufanya kazi hii muhimu na kama anaweza kuanzisha mazungumzo naye (Nyerere),” unasema ujumbe huo wa Rusk.

Inaelekea kwamba mpaka wakati huo ambao Wamarekani walikuwa wakihangaika kuhusu suala la muungano, hakuna Mtanganyika wala Mzanzibari aliyekuwa na mawazo hayo— inawezekana hata viongozi wao wakuu wa nchi hizo.

Siku hiyo hiyo, Machi 14, Frank Carlucci alikuwa na shughuli nyingi visiwani Zanzibar za kuwagonganisha na kuwagombanisha wafuasi wa vyama vya Afro-Shirazi Party (ASP) na Umma Party, ikiwa ni pamoja na kujenga hali ya kutoelewana kati ya wanachama na mashabiki wa vyama hivyo.

Nia yake kubwa ilikuwa ni kuvuruga umoja ulioonyeshwa wakati wa mapinduzi.

Alijua kwamba umoja ulioonyeshwa na Wazanzibari wakati wa mapinduzi ungemzuia kutekeleza kile ambacho CIA ilitaka kifanyike.

Inasadakiwa kuwa Carlucci alikuwa akidodosa taarifa kutoka sehemu tofauti, ikiwa ni pamoja na kujaribu kupata habari kwa njia ya kuwahoji watu mbalimbali, akiwemo katibu mkuu wa ASP, Sheikh Thabit Kombo. Lakini kwa kiasi fulani, Kombo alijua mwelekeo wa siasa za Marekani, ingawa hakujua nia halisi ya Carlucci.

Katika taarifa aliyoituma kwenda Washington, Marekani, Machi 23, Carlucci alisema: “Nimemweleza Thabit Kombo kwa uangalifu mkubwa kuhusu wasiwasi wangu kuhusu namna Wakomunisti wanavyojieneza … Kombo alinijibu kwamba yeye na Sheikh Abeid Karume wanajua ubaya wa tatizo hilo lakini kwa hapa mwanzoni hawapaswi kwenda pupa. Lazima waende taratibu na polepole.

“(Kombo) Alisema alikuwa anachukua hatua moja kwa wakati mmoja na kunidokezea mpango wake wa kumhamisha mfuasi wa Kikomunisti ambaye ni kamishna huko Pemba kwenda kufanya kazi nje ya nchi ikiwa kama mfano wa hatua ambazo Karume anachukua dhidi ya Wakomunisti …Nitaendelea kumbana Kombo na kutafuta mwanya wowote unaoweza kupatikana ili niweze kumpata Karume mwenyewe.”

Awali, Machi 26, Carlucci alizuru Pemba katika harakati zake za siasa. Akiwa Wete. alikutana na Kamishna Diria, Khamis Masoud wa eneo la Mkoani na Ali Sultan Issa wa Chake Chake na alimzungumzia.“Nilikaa siku mbili kama mgeni nyumbani kwa Issa … Issa ni mtu mwenye uwezo, anayeheshimiwa na watu, anayeupenda mno ukomunisti na anayezungumza sana kuhusu siasa za Peking (China, ambako ukomunisti ulikuwa umeenea sana) na alijaribu hata kunishawishi na mimi niwe Mkomunisti,” alisema.

Katika ukurasa wa 95 wa kitabu cha Race, Revolution, and the Struggle for Human Rights in Zanzibar: The Memoirs of Ali Sultan Issa and Seif Sharif Hamad, mwandishi G. Thomas Burgess anasema akiwa Pemba Carlucci alitembezwa na Ali Sultan Issa akitumia gari yake na pia walilala kitanda kimoja kwa sababu mke wa Issa hakuwapo. Na waliongea hadi saa 10:00 usiku usingizi ulipowachukua. Baadaye, Ali Sultan alihamishiwa ubalozi wa Zanzibar mjini London, Uingereza, ikiwa kama sehemu ya kile kilichoelezwa awali kama “hatua moja kwa wakati mmoja” kama mbinu za kukabiliana na chama cha Umma ambacho kilidaiwa kuwa na msukumo mkubwa sana wa siasa za Kikomunisti.

Akimzungumzia Ali Sultan Issa, Carlucci alisema: “Jambo linalotia moyo ni kwamba (Sheikh) Karume amefanikiwa kumuondoa Issa (kutoka Unguja kiasi kwamba) alimkatalia hata kuahirisha safari yake kwa siku moja ili aweze kujiandaa vizuri zaidi.”

Lakini, Dean Rusk alikuwa na wasiwasi uliokuwa ukiongezeka kuhusu kile alichokiita “maendeleo ya polepole” visiwani Zanzibar. Kila sekunde ilikuwa muhimu kwake. Uhakika alioutaka ni kuona kuwa Zanzibar inakuwa salama dhidi ya wakomunisti na kwamba watu wote waliokuwa na damu ya ukomunisti hawangekuwa na nguvu yoyote ya kisiasa.

Alipoona uvumilivu wake kuhusu Zanzibar unaelekea kumshinda, alituma barua ya siri kwa mtu aliyejulikana kama Rab Butler, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, ikiwa ni kama muda usiozidi wiki mbili tangu ziara ya katibu wa Jumuiya ya Madola, Edwin Duncan Sandys.

Katika barua hiyo kwa Rab (Richard Austen Butler) Butler, Rusk alisisitiza tena mambo aliyoyasema awali, na kumalizia kwa msisitizo wa kuanzishwa kwa Zanzibar Action Plan (ZAP), mpango wa kuivamia Zanzibar kutokana na kushindikana kwa muungano.

Yaani machafuko yangepandikizwa Unguja na Pemba na kusababisha taifa au mataifa ya nje yaingilie suala hilo kama njia ya kulipatia ufumbuzi. Kwa waliokuwa wakipanga mipango hiyo, kwao ni heri kungekuwapo machafuko kuliko ukomunisti.

Itaendelea kesho