Marekani yasitisha kuiongezea ushuru China

Wednesday August 14 2019

Washington, Marekani. Serikali ya Marekani imesema itachelewesha ongezeko la ushuru kwa baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na China.

Ofisi ya mwakilishi wa kibiashara wa Marekani ilisema leo Jumatano Agosti 14 kuwa bidhaa ambazo hazitolipwa ushuru ni pamoja na simu za mkononi, kompyuta, viatu na nguo.

Kwa mujibu wa ofisi hiyo, bidhaa hizo zimeondolewa kwenye orodha ya zile ambazo ushuru wake utaongezeka kwa asilimia 10 kuanzia Septemba Mosi.

Hata hivyo, ofisi hiyo ilisema bidhaa zilizosalia zenye thamani ya dola zipatazo bilioni 300 zinazoagizwa kutoka China zitaathiriwa na ongezeko hilo ambalo China inalitaja kuwa sera ya uchokozi wa kibiashara.

Habari za kucheleweshwa kwa ushuru huo zilisababisha kupanda kwa asilimia mbili kwa thamani ya hisa kwenye soko la mitaji la Dow Jones mjini New York.

Duru nyingine ya mazungumzo kati ya China na Marekani inatarajiwa kufanyika mwezi ujao mjini Washington lakini kukithiri kwa mvutano kati ya nchi hizo kumeyatia mashakani mazungumzo hayo.

Advertisement

Advertisement