Masauni aagiza uhakiki kuondoa mlundikano wa wafungwa

Naibu waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamad Masauni akikagua nguo zinazoshonwa na wafungwa kwenye gereza la Butimba Jijini Mwanza ambapo amekagua na kutembelea miradi wa ushonaji unaofanywa na wafungwa. Picha na Johari Shani

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amewaagiza wakuu wa magereza nchini kufanya uchambuzi kubaini wafungwa wenye kesi zinazodhaminika ili kuondoa msongamano

Mwanza. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amewaagiza wakuu wa magereza nchini kufanya uchambuzi kubaini wafungwa wenye kesi zinazodhaminika ili kuondoa msongamano.

Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 12, 2019 wakati akizungumza na maofisa wa Jeshi la Magereza alipotembelea Gereza Kuu la Butimba mkoani Mwanza.

Amewataka maofisa hao kutosubiri viongozi wa kitaifa kutembelea magereza na kuzungumza na wafungwa.

“Timizeni wajibu wenu kwa ajili ya kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu gerezani. Baadhi ya watu wanateseka kwa kuwa mashauri yao ni madogo na yana dhamana,” amesema Masauni.

Akizungumzia msongamano wa wafungwa na mahabusu  Mwanza,  mkuu magereza mkoani humo, Hamza Hamza amesema ingawa uwezo wa kuhifadhi wafungwa na mahabusu kwa magereza zote mkoani humo ni 1, 249, kwa sasa wapo 2,633, ikiwa ni ziada ya watu 1, 384.

“Gereza Kuu la Butimba pekee linahifadhi wafungwa na mahabusu 1, 888 licha ya kuwa na uwezo wa kuhifadhi watu  934,” alisema Hamza