Masauni atoa miezi miwili kwa madereva

Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Injinia Hamad Yusuf Masauni akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa kikao cha Baraza la usalama la Taifa Barabarani kilichofanyika Hoteli ya Ocean View Mjini Unguja, Picha na Haji Mtumwa

Muktasari:

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amewapa miezi miwili madereva wa magari ya abiria, akiwataka hadi Oktoba Mosi, 2019 magari yao yawe yamekaguliwa na kubandikwa stika za uthibitisho

Unguja. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Tanzania, Hamad Masauni amewapa miezi miwili madereva wa magari ya abiria, akiwataka hadi Oktoba Mosi, 2019 magari yao yawe yamekaguliwa na kubandikwa stika za uthibitisho.

Masauni ambaye ni mwenyekiti wa baraza la Taifa la usalama barabarani Tanzania ametoa tamko hilo leo Ijumaa Agosti 9, 2019 katika kikao cha baraza hilo kilichofanyika Unguja, Zanzibar.

Amebainisha kuwa ukaguzi huo ni lazima kwa magari yote, na ambayo yatakosa stika hizo wahusika wote watakamatwa kwa kukiuka agizo hilo.

“Kuepusha usumbufu wananchi wanatakiwa kuyapeleka mapema magari yao kukaguliwa ili kuepusha ajali kutokana na ubovu wa magari,” amesema.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini Tanzania, Forturnatus Muslimu amesema lengo la kikao hicho ni utaratibu wa baraza hilo kufanya vikao kila baada ya muda kwa lengo la kufanya tathmini na kuona utekelezaji wa mpango mkakati umefanyika kiasi gani na mafanikio yake.

Amebainisha  katika mkutano huo walifanya tathmini na kuonyesha ajali za barabarani  Zanzibar zimepungua kwa asilimia 22.5, kwamba hali hiyo inaonyesha kuna mafanikio.

Naye mwenyekiti wa bodi ya mamlaka ya usafirishaji Zanzibar, Mohamed  Simba amesema taasisi yao imejiandaa kuhakikisha madereva wanafuata sheria za barabarani bila shuruti.