Masele kueleza mbivu, mbichi baada ya kikao cha kamati

Dar es Salaam. Mbunge wa Shinyanga Mjini, Stephen Masele amesema baada ya kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya Bunge, atazungumza na waandishi wa habari.

Spika wa Bunge Job Ndugai amemtaka mbunge huyo kufika mbele ya Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge leo saa tano asubuhi kuhojiwa na akikaidi wito huo atakamatwa.

Akizungumza kwa simu jana, Masele alisema, “kwa sasa hivi siko kwenye mazingira ya kuzungumzia hilo jambo, niache kwanza nimalize hicho kikao kisha nitazungumza rasmi na waandishi wa habari,” alisema Masele.

Wiki iliyopita Spika Ndugai alilieleza Bunge kuwa ameamua kumrudisha Masele kutoka katika Bunge la Afrika (PAP) kutokana na utovu wa nidhamu.

“Stephen Masele ni kiongozi ambaye amekuwa akifanya mambo ya ovyoovyo, ndiyo maana tumemuita atufafanulie huenda yuko sahihi, lakini anafanya mambo ambayo ni hatari kubwa, amekuwa akigonganisha mihimili,” alisema Spika Ndugai.

Alisema amemwandikia barua Rais wa PAP ya kusitisha uwakilishi wa Masele katika bunge hilo hadi Kamati ya Maadili itakapokamilisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yake.

Mbali ya kamati hiyo ya Bunge, Ndugai alisema Masele pia atakwenda kuhojiwa na kamati ya Bunge ya chama chake.

Hivi karibuni, Masele ambaye pia ni Makamu wa Rais wa PAP alikaririwa akiwa Afrika Kusini ambako Bunge hilo limekuwa likifanyia mikutano yake, akimtuhumu Rais wa Bunge hilo, Roger Nkodo Dang wa Cameroon kwa rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani (DW) Ijumaa iliyopita, Masele alisema msimamo wa kuunda tume ya uchunguzi ya Rais huyo wa PAP ndicho chanzo cha mgogoro wake na Ndugai.

Wakati wa uchunguzi huo, tayari Masele alikuwa akikaimu nafasi ya Rais wa Bunge hilo, akisema ripoti imeshakamilika na inaonyesha Dang alikuwa na kesi za kujibu.

“Mimi nimeunda tume kumchunguza Rais wa Bunge la Afrika anayetuhumiwa kwa rushwa, matumizi mabaya ya ofisi, undugu, tuhuma za ngono, ripoti (uchunguzi) ilitakiwa iwekwe jana (juzi) ndani ya Bunge na kujadiliwa.”

“Kwa hiyo huyo Rais (Dang) akijua mimi makamu wa kwanza wa Rais na anatambua misimamo yangu, na sipendi mambo ya hovyo hovyo, akaamua kumtumia Spika wetu wa nyumbani ili aweze kuniita haraka nishindwe kuwepo hapa Afrika Kusini kuongoza vikao ambavyo vingejadili ripoti ya uchunguzi, hiyo ndiyo sababu kubwa,” alisema Masele ambaye alikubali kutii agizo la kurejea nchini kwa ajili ya kuhojiwa na kamati mbili zilizoandaliwa ndani ya Bunge .