Mashahidi 30, vielelezo 80 kutumika usikilizwaji kesi vigogo wa Rahco

Muktasari:

  • Serikali inatarajia kuwaita mashahidi 30 na kutumia vielelezo 80 wakati wa usikilizwaji kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa  Kampuni Hodhi ya Mali za Shirika la Reli (Rahco).

Dar es Salaam. Serikali inatawaita mashahidi 30 na kutumia vielelezo 80 wakati wa usikilizwaji kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili vigogo wa Kampuni Hodhi ya Mali za Shirika la Reli (Rahco).

Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji, Benhadard Tito; Mwanasheria wa Rahco, Emmanuel Massawe; na mfanyabiashara ambaye pia ni mwakilishi wa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Limited, Kanji Mwinyijuma.

Wakili wa Takukuru, Maghela Ndimbo amewasomea hoja za awali jana Jumanne Aprili 23, 2019 washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Thomas Simba.

Washitakiwa hao wamepewa nakala za hoja hizo kwa ajili ya kuzipitia wakishirikiana na mawakili wao, baada ya kuzipitia na kuhojiwa na Mahakama walikiri majina yao, vyeo na kwamba waliletwa mahakamani na kusomewa mashtaka huku wakikana mashtaka hayo.

Kwa mujibu wa hoja hizo, inadaiwa mshtakiwa Mwinyijuma ambaye ni raia wa Kenya kati ya Septemba 2014 na Desemba 30, 2015 aliteuliwa na Waziri wa Uchukuzi (wakati huo), Dk Harrisson Mwakyembe kutoa ushauri na mapendekezo yake kwa wizara hiyo na Rahco kuhusu mradi wa ujenzi wa reli ya kati.

Inadaiwa licha ya mambo mengine, mshtakiwa Massawe pamoja na wadhifa wake huo, alikuwa mjumbe wa bodi ya Rahco na alikuwa na mamlaka ya kusimamia mchakato wa kumpata mzabuni na kumsainisha mkataba kwa mujibu wa sheria.

Inadaiwa kati ya Desemba mosi 2014 hadi Desemba 30, 2015 washtakiwa wote waliingia katika mazungumzo kuhusu ujenzi wa reli hiyo na kuielekeza Rahco kupata ushauri kutoka kwa kampuni ya Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji wa reli hiyo kwa gharama ya Dola1.357 milioni bila kushirikisha bodi ya Rahco.

Pia, wanadaiwa kuwasilisha mkataba kati ya kampuni hizo mbili kwa mwanasheria mkuu wa Serikali kwa ajili ya kuupitia na nakala zingine kuzipeleka kwa mamlaka husika kama Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkaguzi wa Ndani na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwamujibu wa sheria.

Februari 27, 2015 kupitia barua EA224/355/01, Tito aliikagua kampuni Rothschild (South Africa) Proprietary Ltd kama mshauri wa mradi wa uimarishaji reli hiyo.

Machi 12, 2015 Tito na Mwinyijuma waliipitisha kampuni hiyo ya Afrika Kusini kuwa mshauri wa mradi wa uimarishaji reli ya kati na kutoa huduma za ushauri wa fedha kuhusu mradi huo bila kushirikisha bodi ya zabuni ya Rahco.

Inadaiwa Mei 20, 2015 washtakiwa hao walisaini mkataba kati ya kampuni hizo mbili kwa gharama ya Dola 1 milioni za Marekani bila kodi wala kuhusisha bodi ya wazabuni ya Rahco na kuuwakilisha mkataba huo kwa mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) kwa ajili ya kuupitia.

Ameeleza kuwa kati ya Machi mosi hadi Septemba 2015, washtakiwa wote walipitisha malipo ya awali ya Dola 500,000 za Marekani kwa kampuni hiyo ya Afrika Kusini na kusababishia Rahco kupata hasara ya Dola 527,540 za Marekani.

Imedaiwa Agosti 18, 2015 Tito kwa wadhifa wake aliipitisha Kampuni ya M/s China Railways Construction Corporation kufanya ujenzi wa reli wa kilomita mbili  eneo la Songa kwa gharama ya Dola 2.31 milioni za Marekani bila idhini ya bodi ya zabuni ya Rahco kinyume cha sheria.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 6 mwaka huu itakapoanza kusikilizwa.