Mashahidi 82, vielelezo 319 kutumika kesi ya aliyetajwa na Magufuli

Muktasari:

Mashtaka 103 ni ya kutoa taarifa za uongo, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh24 bilioni, shtaka moja la kukwepa kodi na jingine la kupanga njama za kukwepa kodi.

Dar es Salaam.Serikali inatarajia kuwaita mashahidi 82 na kutumia vielelezo 319 katika katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mohamed Mustafa Yusufali aliyewahi kutajwa na Rais John Magufuli kuwa anaiibia Serikali Sh7 milioni kwa dakika na wenzeke wawili.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 8 ya mwaka 2019, Yusufali maarufu kwa majina ya Choma, Mohamedali au Mohamed Jamalee na wenzake wawili, Arifal Paliwalla na meneja wa benki ya I&M tawi la Kariakoo, Sameer Khan, wanakabiliwa na mashtaka 544.

Mashtaka hayo ni pamoja na ya kutakatisha fedha, kukwepa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya Sh24 bilioni.

Idadi hiyo ya mashahidi na vielelezo ilitajwa jana na upande wa mashtaka wakati wa hatua ya kufungwa kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na sasa imehamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi au Mahakama ya Ufisadi kwa ajili ya usikilizwaji.

Awali, washtakiwa hao walisomewa upya mashtaka yanayowakabili na jopo la mawakili wa Serikali wanne, kwa zamu lililoongozwa na wakili wa Serikali Mkuu, Pendo Makondo akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi Christopher Msigwa na mawakili wa Serikali Faraja Nguka na Daisy Makakala.

Baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka hayo, Wakili Makondo aliieleza Mahakama kuwa katika kesi hiyo watakuwa na mashahidi hao 82, huku akiwataja kwa majina na vielelezo 319 ambavyo pia amevitaja.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustine Rwizile anayesikiliza shauri hilo aliwauliza mshtakiwa namba moja hadi tatu kama wana kitu cha kuongea kabla ya kesi hiyo haijaenda Mahakama Kuu Kitengo cha Mafisadi, wote walijibu wataenda kuzungumza katika Mahakama hiyo.

“Washtakiwa mmesikia maelezo yote yaliyosomwa, sasa Mahakama hii inawapeleka Mahakama Kuu hivyo mtapewa tarehe ya kusikilizwa shauri hilo,” alisema Hakimu Rwizile na kuamuru washtakiwa hao warudishwe rumande hadi kesi yao itakaposikilizwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika mashtaka hayo 544; mashtaka 102 ni ya utakatishaji fedha, 264 ya kughushi na 72 ya kuwasilisha nyaraka za uongo Mamlaka ya Mapato (TRA).

Mashtaka 103 ni ya kutoa taarifa za uongo, shtaka moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh24 bilioni, shtaka moja la kukwepa kodi na jingine la kupanga njama za kukwepa kodi.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo kwa nyakati tofauti kati ya Januari 2008 na Januari 2016 katika jijini la Dar es Salaam.

Inadaiwa katika kipindi hicho Yusufali akiwa mkurugenzi wa kampuni ya Farm Plant Ltd iliyosajiliwa kulipa VAT, kwa nia ya kukwepa kodi, aliwasilisha makadirio ya kodi ya uongo kwa kamishna wa TRA hivyo kukwepa kulipa kodi ya Sh24 bilioni.