Masharti ya kampeni yambana Mrisho Mpoto, sasa kuvaa viatu

Saturday May 25 2019

 

By Phinias Bashaya, Mwananchi [email protected]

Bukoba. Bila shaka unamfahamu msanii maarufu nchini, Mrisho Mpoto jinsi anavyoimba mashairi yake maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi huku akiwa hajavaa viatu.

Safari hii atalazimika kuvaa viatu kutokana na kubanwa na masharti ya Wizara ya Afya katika kampeni yake ya ‘Nyumba ni Choo’ iliyozinduliwa leo Jumamosi Mei 25, 2019 kwa Mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mratibu wa kampeni ya kitaifa ya usafi wa mazingira,  Anyitike Mwakitalima amesema leo mjini Bukoba kuwa msanii huyo anatakiwa kuchagua moja ili aendelee kuwa na sifa za kushiriki kampeni hiyo.

Amebainisha wizara hiyo ina miiko na taratibu zake zinazoendana na usafi wa mazingira na haiwezi kuwa sahihi kumtumia msanii asiyevaa viatu kwa kuwa hatua hiyo inaleta uwezekano wa kuambukizwa magonjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mratibu huyo amesema kampeni hiyo itafika hadi vijijini, akisisitiza ni lazima Mpoto avae viatu.

Kwa upande wake Mpoto amesema anakubaliana na sharti hilo na kubainisha kuwa si kwa sababu anapenda pesa bali kuunga mkono juhudi za Serikali.

Huku akicheka amesema suala la yeye kutovaa viatu limekuja ghafla ni kama hakushirikishwa mapema.

Kampeni hiyo kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa inazindiliwa leo katika uwanja wa Kaitaba.

Advertisement