Masikini milioni moja waongezeka Tanzania

Muktasari:

Ingawa uwiano umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2007 hadi asilimia 26.8 mwaka 2016, idadi ya mafukara imeongezeka kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu. Zaidi ya watoto milioni mbili huzaliwa kila mwaka nchini.


Dar es Salaam. Kwa miaka mitano, 2012 hadi 2016, Benki ya Dunia imesema mafukara milioni moja wameongezeka nchini Tanzania.

Juhudi za kukuza uchumi, benki hiyo imesema ni ndogo ikilinganishwa na kasi ya ongezeko la watu. Juhudi hizo zimefanikisha kushusha uwiano wa masikini kutoka asilimia 34.4 ambao ni sawa na milioni 13.2 mwaka 2007 hadi asilimia 26.8 sawa na milioni 13.3 mwaka 2016.

Lakini, “idadi ya wanaoishi chini ya mstari wa umasikini wameongezeka kutoka milioni 12.3 mwaka 2012 sawa na asilimia 28.2 hadi milioni 13.3 sawa na ongezeko la mafukara milioni moja,” inasomeka sehemu ya ripoti ya Benki ya Dunia.

Hilo limebainishwa leo, Julai 18, 2019 Benki ya Dunia ilipozindua ripoti ya 12 ya hali ya uchumi Tanzania iliyoangazia umuhimu wa rasilimaliwatu katika kukuza utajiri.

 

Ingawa Serikali inawekeza kuimarisha miundombinu hasa ya elimu, usafiri na usafirishaji pamoja na afya, mchumi mwandamizi wa benki hiyo, Bill Battaile amesema maisha ya wananchi bado si mazuri.

Mchumi huyo amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo utajiri (wealth) wa wananchi wake umeshuka ndani ya miongo miwili iliyopita.

Kushuka kwa utajiri huo kumeongeza idadi ya mafukara wanaoishi chini ya Dola moja kwa siku nchini ambayo ilifika milioni 13.3 mwaka 2018 ikilinganishwa na milioni 12.3 waliokuwapo mwaka 2012.

Pamoja na hayo, Battaile alisema: “Mwaka 1995 wastani wa utajiri wa kila Mtanzania ulikuwa Dola 20,900 lakini mwaka 2014 umeshuka mpaka Dola 17, 451.”