UCHAMBUZI: Matamko ya matumaini kuelekea uchaguzi 2020

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Muktasari:

Mawaziri waliofanya ziara Bwawa la Mindu kwa wakati mmoja ni William Lukuvi, ambaye ni Waziri wa Ardhi, Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi), Profesa Makame Mbarawa (Maji), Suleiman Jafo (Tamisemi), Hamis Kigwangalla (Maliasili na Utalii), Hussein Mwinyi (Ulinzi), Omari Mgumba (Naibu Waziri wa Kilimo) na Mussa Sima (Naibu Waziri wa Mazingira).

Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesimamisha utekelezwaji wa mpango wa kuwahamisha wananchi wanaoishi kando ya Bwawa la Mindu, hatua ambayo wachambuzi wameielezea kuwa ni ya kawaida kabla ya Uchaguzi Mkuu.

Lukuvi alitoa tamko hilo wakati wa ziara iliyohusisha mawaziri wanane waliotembelea bwawa hilo kuangalia changamoto ya sheria inayozuia watu kufanya shughuli zao na kuweka makazi ndani ya mita 60 na 500 kutoka mabonde ya mito na mabwawa.

Bwawa hilo linachangia asilimia 80 ya maji yanayotumika mkoani Morogoro, lakini wataalamu wanasema uwepo wa makazi ya watu na shughuli zao, kama uchimbaji madini, umesababisha kina chake kupungua na hivyo kutishia kuendelea kwa huduma hiyo.

Lakini Waziri Lukuvi akatoa tamko tofauti na maoni ya wataalamu hao.

“Tumesikia wataalamu walichosema ila tunaagiza hatua zozote zisichukuliwe hadi mtakapopata maelekezo kutoka kwa waziri mwenye dhamana,” alisema Waziri Lukuvi baada ya kusikia maelezo kutoka kwa ofisa wa maji ya Bodi ya Bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani

“Tumesikia mlitaka kuwahamisha wakazi hawa wiki ijayo, msiwatoe.”

Tamko hilo ni moja ya matamko kadhaa ambayo wachambuzi wamesema hutolewa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, wakionya wananchi kuwa waangalifu kwa kuwa sheria hufuata mkondo wake mara baada ya kipindi hicho kuisha.

Walisema matamko mengine huhusu mambo kama ahadi za kuongeza mshahara kwa wafanyakazi, kuzuia kwa muda utekelezwaji wa kubomoa nyumba zilizojengwa maeneo yaliyozuiwa, ahadi za mikopo na vitendea kazi kwa wafanyabiashara wadogo na mengine ya kuwapunguzia kero wananchi.

Lakini wachambuzi waliohojiwa na Mwananchi wanasema hali hiyo hutokea kila wakati uchaguzi unapokaribia, lakini baada ya uchaguzi mambo hurudi palepale.

“Fikra hizi za kuwaonea huruma wananchi zimekuja wakati huu kwa sababu kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na (hayo) ndiyo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao,” alisema mpigania haki za binadamu nchini, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema.

Alisema watendaji wanajua wananchi wanaosumbuliwa ndio wapigakura wao, hivyo wanatafuta namna ya kuwa karibu nao.

“Kwa mfano, imezoeleka kipindi kama hiki wamachinga wanaachwa watawanyike wanavyotaka. Baada ya uchaguzi wanapumzika kidogo, (lakini) baadaye huanza kufurushwa,” alisema mkurugenzi huyo wa zamani wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Alisema kama Serikali imeruhusu wananchi kuendelea kuishi na kufanya shughuli zao kando ya vyanzo vya maji, mito na mbuga za wanyama, itakuwa tayari kuwafidia wananchi ambao awali walibomolewa nyumba zao na kuharibiwa mazao yao awali.

“Kuna waliovunjiwa nyumba zao na hawakuwa na elimu ya kutosha kuhusu kujenga maeneo yasiyo rasmi. (Hawa) Wanafidiwa vipi?” alihoji Bisimba.

“Walio kwenye maeneo yasiyo rasmi wasibweteke. Wajipange (kwa kuwa) baada ya uchaguzi wanaweza kujikuta wakipata taabu tena.”

Maoni kama hayo yalitolewa na rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume, ambaye alisema kuna mambo yanatolewa matamko bila ya kuwa na mashiko ya kisheria.

Alisema maeneo kama ya hifadhi za Taifa, mbuga za wanyama, vyanzo vya maji, yapo kisheria na yanalindwa kwa mwongozo wa sheria. “Kutamka tu kwamba wananchi waendelee (kuishi), itakuwa ni kwa muda,” alisema wakili huyo wa kujitegemea na mwanaharakati wa sheria.

“Akija kiongozi mwingine au baada ya uchaguzi zitatumika sheria hizo kikamilifu na hakuna atakayepinga.”

Alisema kufanya hivyo kunamaanisha watendaji au watawala hawataki kuzitumia sheria walizozitunga.

“Ndiyo linakuja swali wanafanya kazi kwa utawala wa sheria au matakwa ya mtu?” alihoji.

“Kwa nini yanabadilika wakati huu? Matamko haya hayawezi kuwa ya kudumu hadi zile sheria zibadilishwe. Kinachoendelea sasa ni sawa na danganya toto. Uchaguzi ukiisha watarudi kwenye sheria na kuwabadilikia wananchi, hivyo badala ya kuchekelea, wanatakiwa pia wadai uhakika wa kudumu kisheria.”

Dk Richard Mbunda, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anaona kuna ajenda nyuma ya matamko hayo.

“Kinachoendelea sasa kufuatia matamko hayo yenye mrengo wa kuwahurumia wananchi ni kama kutaka kuahirisha tatizo kwa sababu sheria, kanuni na taratibu zipo vile vile,” alisema.

“Huu ni mkakati wa kisiasa kujaribu kuwapooza wapigakura wa makundi mbalimbali kuonyesha kuwa inawajali.”

Alisema matamko hayo aliyoyaita ya kubadili upepo, yanatolewa kwa kada zote za wakulima, wafugaji, wafanyakazi na wafanyabiashara.

Dk Mbunda alisema baadaye makundi hayo yataona kama Serikali ipo upande wao na inawajali wakati kuna sheria na kanuni zinazopaswa kufuatwa katika kila jambo na kuzikiuka ni kosa.

“Mkakati huu unaweza kufanikiwa na wakashinda tena uchaguzi ujao kwa sababu wapigakura ni hawa wananchi wa kada hizi wanazozigusa,” alisema.

Alisema baadhi ya viongozi wanaotoa matamko hayo hawaonyeshi hata kama kuna sheria, kanuni mpya zinatungwa ili kubadili zile zilizokuwepo awali kwa sababu malengo yao ni ya kisiasa.

“Kama wanavunja sheria, huko mbele itakuja kuchukua mkondo wake. Huwezi kujenga kwenye hifadhi ya barabara na sheria ikakuacha. Watu hawawezi kupona kwa namna yoyote ile,” alisema Dk Mbunda.

Naye mkurugenzi mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema anaona kuna mambo mawili ambayo viongozi Serikali wanayafanyia kazi, ikiwa ni mkakati wa kujaribu kurudisha imani ya nchi kimataifa baada ya malalamiko mengi dhidi ya kuminywa kwa haki za binadamu.

“Mashirika mengi ya kimataifa yamekuwa yakilalamika na ukiangalia ni kweli kuna baadhi ya maeneo wananchi wanaishi kama wakimbizi nchini mwao,” alisema.

“Jambo la pili ni mwakani kuna uchaguzi mkuu, masuala kama ya kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura, kampeni ndogondogo zimeanza na wanajua kutakuwa na hekaheka ya kutaka kibali kwa wananchi, hivyo lazima wawatulize kupitia yale waliyoyafanya kuwaumiza.”

Alisema kwa miaka kadhaa wauzaji vyakula, maarufu kama mama ntilie, wamekuwa wakisumbuliwa lakini ukikaribia uchaguzi huachwa wafanye shughuli zao lakini baada ya muda husumbuliwa tena.

“Jukumu la wananchi ni kutoshangilia matamko ya mdomo, bali kuomba mabadiliko yafanyike kisheria; kuanzia kwenye sera , kanuni na taratibu za utendaji,” alisema.