Matapeli watumia simu kuliza wazazi

Monday February 11 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Zama za kutumia silaha kama bunduki, mapanga au visu kuvamia makazi ya watu hivi sasa ni kama zimepitwa na wakati kutokana na teknolojia ya mawasiliano kuja na mabadiliko hasi.

Licha ya manufaa yanayoyapatikana kutokana na ujio wa mawasiliano hayo, wahalifu nao wanayatumia kinyume chake kwa utapeli.

Kwa mfano mzazi anapigiwa simu na mtu asiyejulikana akijitambulisha kuwa ni mwalimu anamuarifu kwamba mtoto wake yupo hosiptali.

Wakisimulia yaliyowahi kuwakuta kutokana na teknolojia hiyo, mkazi wa Makumbusho, Mwanaisha Issa akiwa kwenye daladala akitokea Mbagala kuelekea Magomeni alipigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwalimu na kumweleza kuwa mtoto wake mwanafunzi wa darasa la tatu yupo mahututi Kituo cha Afya Arafa Magomeni.

Mwalimu huyo ambaye hakujitambulisha jina alimuomba Mwanaisha kutumia Sh45,000 kwa ajili ya dawa kwani akichelewa mtoto wake anaweza kupoteza maisha.

“Tafadhali mwalimu naomba msaidie mwanangu nipo njiani nakuja simu yangu haina hela ila nashuka muda si mrefu nipo kwenye daladala, nakuomba tafadhali,” alisikika mama huyo aliyegubikwa na huzuni usoni akiwa kwenye daladala.

Hata hivyo, abiria waliokuwa kwenye daladala walimshauri Mwanaisha kupiga simu nyumbani ili kuomba msaada, lakini baada ya kupiga simu alielezwa kuwa mtoto yupo nyumbani salama.

Mkazi wa Tegeta, Victoria James naye alisema alishakumbwa na tatizo hilo na kulazimika kutuma Sh100,000 baada ya kupigiwa simu na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwalimu.

“Huu ni utapeli wazazi wengi wanalalamika kupigiwa simu na walimu kuwa mtoto anaumwa ili utume hela, ukituma anazima simu,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mabel Masasi alipoulizwa kuhusiana na jambo hilo alisema polisi ndiyo wenye mamlaka ya kutolea ufafanuzi.

Alipoulizwa msemaji wa Polisi nchini, Ahmed Msangi aliwatahadharisha wazazi kuwa makini kwani wezi wanaangalia njia ambayo wanaweza kupata fedha kwa rahisi.

Advertisement