Matawi ya CUF Pemba yatimkia ACT-Wazalendo

Muktasari:

  • Mwananchi ilishuhudia baadhi ya matawi ya Pemba yakishusha bendera hizo na aliyekuwa mwenyekiti wa CUF wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid alisema matawi zaidi ya 404 ya Pemba yamekubaliana kumuunga mkono Maalim Seif.

Pemba. Wakati Maalim Seif Sharif Hamad na viongozi wengine wakikabidhiwa kadi ACT-Wazalendo, maeneo mbalimbali ya Zanzibar jana yalikuwa yakishusha bendera za CUF.

Na hawakuishia hapo, walianza kupandisha bendera za ACT-Wazalendo na katika baadhi ya maeneo kupaka majengo rangi za chama hicho.

Kutokana na hatua hiyo, bendera za ACT-Wazalendo zimegeuka lulu visiwani hapa kutokana na matawi yaliyokuwan ya CUF kuzihitaji, kama ilivyokuwa kwa baadhi ya matawi mkoani Tanga na Lindi.

Wakati hayo yakijiri, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alikemea vitendo vya kuchoma bendera vinavyofanywa na watu wanaodaiwa kumuunga mkono Maalim Seif.

“Natumia fursa hii kuwaasa wanachama na mashabiki wote wa vyama vya siasa kuepuka kujihusisha na vitendo vyote vya uvunjifu wa sheria. Wakifanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria wao binafsi na vyama vyao,” alisema Jaji Mutungi.

Mwananchi ilishuhudia baadhi ya matawi ya Pemba yakishusha bendera hizo na aliyekuwa mwenyekiti wa CUF wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid alisema matawi zaidi ya 404 ya Pemba yamekubaliana kumuunga mkono Maalim Seif.

Rashid alisema katika wilaya yake kuna matawi 92 ambayo kwa sasa yamegeuka kuwa ya ACT-Wazalendo na miongoni mwa matawi hayo yanaonekana kuwa na bendera za chama hicho.

Aliyekuwa katibu wa CUF wilaya ya Wete, Riziki Omar Juma alisema kuna matawi yasiyopungua 112 ambayo yameridhia kubadilika na kuwa ya ACT-Wazalendo.

Kwa upande wake, aliyekuwa mwenyekiti wa CUF wilaya ya Chakechake, Saleh Nassor Juma alisema kila kitu kinawendea vizuri kama mkakati huo ulikuwa umeratibiwa miaka mitano iliyopita.

Alisema anachokiona ni kwamba ACT-Wazalendo itakuwa na nguvu zaidi kuliko CUF kutokana msuguano wa kiuongozi ambao anadai umekididimiza chama hicho.

Saleh alisema katika matawi 96 ya wilaya yake, wanachama wameridhia kujiunga na chama kipya alichohamia Maalim Seif.

Tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani, CUF imekuwa chama kikuu cha upinzani Zanzibar.