Matiko akumbushia kauli ya wakurugenzi kutowatangaza wapinzani

Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema) Esther Matiko amesema kuna kauli iliyomnukuu Rais John Magufuli kuhusu matokeo ya uchaguzi kwa wapinzani inapaswa kukanushwa

Dodoma. Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema) Esther Matiko amesema kauli aliyonukuliwa Rais John Magufuli kuhusu wakurugenzi kutowatangaza wapinzani, haijafutwa hivyo italeta shida kwenye uchaguzi.

Matiko ameliambia Bunge leo Ijumaa Aprili 12, 2019 wakati akichangia hotuba za ofisi ya Rais Tamisemi na utawala bora.

Matiko amesema wakati Watanzania wakijiandaa kwenda kwenye uchaguzi, bado kuna sintofahamu kuhusu kauli hiyo ambayo amesema italeta machafuko nchini

"Hakuna Rais ambaye aliwahi kusema kuwa upinzani chagua kazi nyingine, lakini huyu amesema na kunukuliwa lakini haijafutwa popote, hapo ndipo shida inapoanzia," amesema Matiko.

Amesema wakurugenzi wengi ambao ndiyo maofisa wa Tume ya Uchaguzi majimboni ni makada wa Chama cha Mapinduzi hivyo si rahisi kutenda haki kwa wapinzani.

Kwa mujibu wa Matiko, ni vema wakachaguliwa makada wa CCM kuwa wakuu wa wilaya lakini siyo wakurugenzi wa halmashauri kwani wanadumaza maendeleo.

Mbunge huyo amesema ni wakati wa Serikali kuangalia juu ya utawala bora kwani eneo hilo bado lina changamoto kubwa.