VIDEO: Matumaini mapya kwa aliyepofushwa macho Kibiti

Dar es Salaam. Matumaini ya kuanza kuona tena yamemsukuma Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu kujitosa kumsaidia Michael Buchayandi ili aweze kupona walau jicho moja, baada ya kupatwa na upofu.

Mgalu, mbunge wa viti maalumu mkoani Pwani amejitosa kusaidia kutafuta wataalamu watakaoweza kunusuru jicho la Buchayandi aliyenusurika wakati wa matukio ya mauaji yaliyofanyika Kibiti mkoani Pwani 2017.

Buchayandi ambaye ni mwenyekiti wa kitongoji cha Rondo wilayani humo, alishambuliwa usiku wa Juni 27, kwa kupigwa risasi na rungu na kusababishiwa majeraha huku akiharibiwa macho na nyumba yake kuchomwa moto.

Kutokana na hali hiyo, hana makazi maalumu na anasumbuliwa na macho ambayo licha ya kushindwa kuona yanamsababishia maumivu makali.

Akizungumza kwa simanzi, Buchayandi alisema ingawa alishambuliwa muda mrefu uliopita, bado anapata maumivu makali kwenye macho na muda wote yanatoa machozi.

Mkewe, Selina Mponye alisema katika mizunguko yao kwenye hospitali mbalimbali wamepewa matumani kuwa upo uwezekano wa jicho moja kupona.

Alisema kilichowafanya washindwe kutibiwa ni gharama za matibabu zinazofikia Sh7 milioni ambazo hawana uwezo wa kuzipata.

“Naumia kumuona mume wangu katika hali hii, tumehangaika sana lakini tumepewa matumaini kwamba anaweza kuona jicho moja, kwangu hilo linatosha.” alisema Selina.

“Akiona hata jicho moja maisha yanaweza kuendelea siyo kama alivyo sasa.”

Alisema, “naomba Watanzania watusaidie, nimeambiwa kuna hospitali Mbeya na gharama yake ni Sh7 milioni, tukiweza kupata fedha hizo tutakwenda kujaribu huenda maisha yetu yakarejea kuwa kama yalivyokuwa zamani.”

Mgalu afungua pazia

Akizungumzia hilo, Mgalu alisema amekuwa akiifuatia familia hiyo kwa muda mrefu, lakini taarifa za kwamba Buchayandi anaweza kuona zimeongeza matumaini.

“Hilo likishathibitishwa na wataalamu tuanze sasa kuhangaikia matibabu, niwaombe Watanzania wote kwa ujumla tuwe pamoja katika hili,” alisema Mgalu.

“Huyu ni mwenzetu anahitaji msaada wetu, yeye ni baba wa familia, watoto wanamtegemea lakini tazama maisha yao yalivyobadilika baada ya tukio hilo, niwaombe kwa namna yoyote tutakavyoguswa tuweze kuwasaidia.”