Matumizi ya gesi yabadili maisha kwa dereva wa Uber

Saturday June 1 2019

Dereva wa Uber anayetumia gari aina ya IST

Dereva wa Uber anayetumia gari aina ya IST jijini Dar es Salaam, Linus Rugemalira 

By Kelvin Matandiko, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Dereva wa Uber anayetumia gari aina ya IST jijini Dar es Salaam, Linus Rugemalira amesema kipato chake kimeongezeka ghafla kwa makadirio ya Sh30,000 kwa siku baada ya kubadili mfumo wa matumizi ya nishati katika gari lake, kutoka mafuta na kutumia gesi asilia ya kujaza.

Rugemalira aliyeanza kufanyabiashara ya kubeba abiria kwa kibarua cha mtandao wa Uber jijini la Dar es Salaam, amesema kabla ya kuunganisha gari hilo na mfumo wa gesi alikuwa akitenga takriban  Sh5,000 kati ya Sh100,000 alizokuwa akikusanya kwa siku kwa ajili ya mafuta. Hufanya mizunguko yake kwa makadirio ya kilomita 160 kwa siku.

“Miezi sita imetimia sasa tangu nitumie gesi, natumia  Sh14,000 kujaza gesi kila siku Ubungo kwa hiyo ninabakiwa na mapato ya karibu Sh80,000 kila siku ikilinganishwa na makadirio ya Sh50,000 niliyopata wakati nikitumia mafuta,” amesema Rugemalira jana jijini Dar es Salaam wakati wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Kanuni za bei ya gesi asilia za mwaka 2016, zinaonyesha matumizi ya gesi hiyo katika magari husaidia kuokoa asilimia 40 ya gharama inayotumika kununua lita moja ya petroli na dizeli ya wakati husika. Hii ni sawa na kupunguza Sh40 katika Sh100 inayotumika katika mafuta ya kiwango hicho.

Kwa mujibu wa TPDC, takriban magari 200 yanaendelea kutumia gesi nchini yakitumia kituo cha kujaza gesi kilichopo Ubungo baada ya kuunganishiwa mfumo huo na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).

“Madereva wenzangu baadhi walikuwa na hofu mwanzoni wanasema gesi italipua gari, mara sijui nini lakini sijawahi kuhisi wala kupata tatizo hilo, kwanza imenisaidia sana kimaisha kuongeza kipato changu, nimefanya service (matengenezo) ndogo mara mbili tu isiyokuwa na malipo pale DIT kwa hiyo mabadiliko ni makubwa wala si uongo,” amesema.

Advertisement

Aprili mwaka huu TPDC, ilianza mazungumzo na mradi wa mabasi yaendayo haraka katika Jiji la Dar es Salaam (Dart), ili kuwezesha mabasi yaendayo kasi takriban 300 kutumia nishati ya gesi asilia.

Advertisement