Mavunde aahidi kuwasaidia vijana wa kampuni ya Agri Ajira, KCL

Muktasari:

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde amesema atawasaidia vijana waanzilishi wa kampuni ya Agri Ajira na KCL kupata maeneo ya kilimo, mikopo na mitaji

Morogoro. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde ameahidi kushughulikia changamoto ya upatikanaji wa maeneo ya kilimo, mikopo na mitaji kwa vijana walioanzisha kampuni ya Agri Ajira na KCL
Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 11, 2019 mkoani Morogoro katika mkutano uliowahusisha vijana wanaounda kampuni hizo.
Mavunde alitoa ufafanuzi huo baada ya kuelezwa na vijana hao kuhusu changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa maeneo ya kilimo, uwezeshwaji katika pembejeo za kilimo na mikopo.
Mavunde aliyekuwa mgeni rasmi katika mkutano huo ameahidi kushughulikia changamoto hizo kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) ili kuwawezesha vijana.
Pia, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kutenga maeneo kwa ajili ya vijana ili kuhakikisha kilimo kinaleta tija kwa kupunguza umasikini kwa watu kujiajiri na kujipatia kipato.