Mavunde atumia siku ya wapendanao kuwatembelea wajawazito

Thursday February 14 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Anthony Mavunde ameitumia siku ya wapendanao ambayo huadhimishwa kila Februari 14, kuwatembelea wajawazito na kuwapa vifaa vya kujifungulia vyenye thamani ya Sh8milioni.

Naibu Waziri huyo katika ofisi ya Waziri Mkuu ametoa vifaa hivyo leo Alhamisi Februari 14, 2019 akibainisha kuwa siku hiyo ni muhimu kwa wenye mahitaji mbalimbali.

Mbali na vifaa 350 vya kujifungulia, ametoa mashuka 100 huku akiahidi kuendeleza kuwasaidia.

“Upendo wangu ni kuwajali wenye mahitaji maalumu hasa ninyi mama zangu, kumbukeni baadhi huwa wanakosa vifaa wakati wa kujifungua ndiyo maana nimewaletea mifuko 350 yenye vifaa vyote vya kujifungulia ambapo mfuko mmoja ni sawa na Sh21,000 pia nawapeni mashuka 100 pamoja na maji kwa ajili ya wagonjwa hapa,” amesema Mavunde.

Amewakumbusha wenye dhamana kuwasaidia watu kadri ya mahitaji na uwezo wao kwani ahadi zao kwenye uchaguzi huwa ni kuwajali watu wa hali ya chini.

Mganga wa Jiji la Dodoma, Dk Gatete Mahava amesema Dodoma kuna jumla ya vituo 91 vinavyotoa huduma ya afya na kati ya hivyo 47 vinatoa huduma ya kuzalisha.

 

 


Advertisement