Mavunde awatoa hofu wakazi wa Mjimwema mkoani Dodoma

Muktasari:

Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Anthony Mavunde amewataka wakazi wa  Mjimwema kata ya Chang'ombe jijini Dodoma  kuwa watulivu wakati mgogoro wa ardhi katika eneo hilo ukifanyiwa kazi.

 


Dodoma. Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), Anthony Mavunde amewataka wakazi wa  Mjimwema kata ya Chang'ombe jijini Dodoma  kuwa watulivu wakati mgogoro wa ardhi katika eneo hilo ukifanyiwa kazi.

Naibu Waziri huyo wa Ofisi  ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Julai 9, 2019 katika uzinduzi wa Shina la wakereketwa wa CCM uliofanyika katika eneo la Soko la Mavunde-Chang'ombe.

"Hivi sasa Mkuu wa Mkoa ameunda kamati inayoendelea kukamilisha baadhi ya taratibu, naomba tusubiri wakamilishe zoezi hili na kama kutakuwa na upungufu utakaojitokeza sisi viongozi wenu tupo tutasaidia kuyatatua, cha msingi ile kero tayari hatua zimeanza kuchukuliwa,” amesema Mavunde.

Kuhusu mikopo amewaahidi wananchi na wafanyabiashara wa kata hiyo kuwa atashirikiana na viongozi wenzake kuwasaidia wenye vikundi wapate mikopo kutoka Halmashauri ya Jiji pamoja na mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi.