Mawakili kuwatetea waliohukumiwa maisha kwa kuchoma moto kituo cha polisi

Muktasari:

  • Jana Ijumaa, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wanane kati ya 18 baada ya kuwatia hatiani kwa makosa ya kuchoma moto kituo cha polisi Bunju A jijini Dar es Salaam mwaka 2015.

Dar es Salaam. Mawakili watano akiwamo Jebra Kambole wiki ijayo watakata rufaa kupinga hukumu ya maisha jela iliyotolewa kwa washtakiwa wanane waliotiwa hatiani katika kesi ya kuchoma moto Kituo cha Polisi cha Bunju A jijini Dar es Salaam.

Jana Ijumaa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam iliwahukumu kifungo cha maisha jela washitakiwa hao huku wengine 10 wakiachiwa huru.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 23, 2019, Kambole amesema watachukua uamuzi huo wiki ijayo baada ya kupata nakala ya hati ya mashtaka ambayo wanategemea kuipata kuanzia Jumatatu ili kuchambua sababu za kukata rufaa.

“Kwa sasa tunaendelea kufanya mawasiliano na wakili aliyekuwa akisikiliza shauri hilo na tunategemea wiki ijayo ku-file notice (kuandaa jalada) ya kukata rufaa kwa sababu bado kuna haki ya kukata rufaa, tunasubiri uamuzi (nakala ya hukumu) ili kujua sababu za rufaa zitakuwa ni nini,” amesema.

Pamoja na mpango huo, Kambole amesema mawakili hao pia wanajaribu kuangalia uwezekano wa kufungua maombi ya kuomba dhamana au kushikilia uamuzi wa mahakama hiyo.

“Wakati tunasubiri rufaa, kuna uwezekano wa kuomba dhamana huku tukisubiri dhamana isikilizwe,” amesema.

Kambole amesema washtakiwa hao wamepewa adhabu hiyo kwa mujibu wa kanuni ya adhabu kifungu cha 319 ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura 16 kama ilivyorejewa mwaka 2002.

Hata hivyo, Kambole amesema Sheria ya Mtoto namba 21 ya 2009, inayomtambua mtoto ni yule mwenye umri chini ya miaka 18, inaelekeza asipatiwe hukumu ya kupelekwa gerezani.

“Lakini hadi tutakapopata hukumu ndiyo tutajua miaka iliyokuwa inaongelewa ilikuwa ni mingapi,” amesema Kambole.

Kwa mujibu wa sheria, mshtakiwa anahukumiwa kwa kuzingatia umri aliokuwa nao wakati akitenda kosa. Lakini siwezi ku-confirm exactly hadi nitakapopata hati ya mashtaka, siwezi kuzungumza kitu ambacho sina uhakika nacho.

Jumla ya washitakiwa katika kesi hiyo walikuwa 35, awali Mahakama ilikwishawaachia huru 17 na kubaki 18 ambapo wanane ndio wametiwa hatiani.

Washitakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na makosa sita ikiwemo kuchoma kituo hicho moto Julai 10 mwaka 2015.

Hukumu hiyo ilisomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, akisema kitendo walichofanya washitakiwa ni unyama kwa kuchoma moto kituo hicho.