Mawaziri washuhudia changamoto utunzaji wa mazingira bwawa la Mindu

Muktasari:

Mawaziri wanane  wamefanya ziara katika bwawa la Mindu kuangalia changamoto ya sheria ya mita 60 na mita 500 kwa makazi na shughuli za binadamu zinazoendeshwa jirani na bwawa hilo

 


Dar es Salaam. Mawaziri wanane  wamefanya ziara katika bwawa la Mindu kuangalia changamoto ya sheria ya mita 60 na mita 500 kwa makazi na shughuli za binadamu zinazoendeshwa jirani na bwawa hilo.

Mawaziri hao ni William Lukuvi (Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi),   Waziri wa Mifugo na Uvuvi,  Luhaga Mpina; Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa,  Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo.

Wengine ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla; Waziri wa Ulinzi, Dk Hussein Mwinyi;  naibu Waziri wa Kilimo,  Omari Mgumba na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazinira),  Musa Sima.

Bwawa hilo ambalo linachangia asilimia 80 ya maji yanayotumika katika Mkoa wa Morogoro linazungukwa na makazi ya watu, limeanza kupungua kina chake kutokana shughuli mbalimbali za binadamu ikiwemo uchimbaji wa madini.

Ofisa wa Maji ya Bodi ya Bonde la Wami Ruvu, Simon Ngonyani amesema uwepo wa wakazi hao unachangia pia kuchelewa kwa mradi wa kuongeza kina cha bwawa hilo.

“Shughuli zinazofanyika ni hatari kwa ustawi wa bwawa, watu wanachenjua madini kwa kutumia Mercury mwisho wa siku inakuja bwawani, wengine wanatumia mbolea zenye kemikali isiyofaa,” amesema Ngonyani.

Lukuvi, ambaye ni mwenyekiti wa timu hiyo maalum ya mawaziri inayoangazia namna ya kutatua migogoro ya uvamizi unaotokana na ardhi na hifadhi amesema bado wanaangalia namna ya kufanya kuhusu mgogoro huo.

“Tumesikia wataalam walichosema ila tunaagiza hatua zozote zisichukuliwe hadi mtakapopata maelekezo kutoka kwa waziri mwenye dhamana, tumesikia mlitaka kuwahamisha wiki ijayo msiwatoe,” amesema Lukuvi.