Mawaziri watatu wajibu hoja ya mishahara

Muktasari:

Mhagama alisema Serikali itakaa na vyama vya upinzani kujadili suala hilo na kwamba, hakuna tatizo lolote.

Dodoma. Mawaziri watatu juzi walijibu hoja ya mbunge wa viti maalumu (Chadema), Ruth Mollel aliyeibana Serikali akitaka iwaongezee mishahara watumishi wa umma kwa kuwa ni haki yao ya kisheria.

Ruth, katibu mkuu mstaafu wa Utumishi, alisema tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani haijawahi kuongeza mishahara ya watumishi.

Hata hivyo, wakijibu hoja hiyo mawaziri hao, George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora), Jenister Mhagama (Ofisi ya Waziri Mkuu) na Naibu Waziri wa Elimu, William Ole Nasha walisema suala hilo Serikali inalijua na italitekeleza wakati ukifika.

“Unataka standard gauge, kukarabati kwanza uwanja wa ndege. Muda utakapofika tutatoa nyongeza mishahara. Walio na dhiki na uwanja wa ndege wangesema tupe ndege kwanza,” alisema Mkuchika

Mhagama alisema Serikali itakaa na vyama vya upinzani kujadili suala hilo na kwamba, hakuna tatizo lolote.

“Tuna muda wa kukaa kujadiliana, Serikali itatekeleza kila jambo kwa
wakati sahihi,” alisema.