Mazungumzo ya jeshi, raia Sudan yakwama

Thursday May 16 2019

 

Khartoum.Sudan. Viongozi wa kijeshi Sudan wamesitisha kwa saa 72 mazungumzo na waandamanaji juu ya kuunda baraza huru la mpito nchini humo.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye televisheni nchini humo, Baraza la Mpito la Kijeshi (TMC) limetoa sharti la kuondoa vizuizi vilivyowekwa na waandamanaji katika maeneo mbalimbali mjini Khartoum.

Duru zinasema hakuna tarehe mpya iliyotangazwa kwa ajili ya mazungumzo juu ya wajumbe wa utawala utakaoliongoza taifa hilo katika kipindi cha mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.

Jumatano watu tisa walijeruhiwa wakati wanajeshi wa Sudan walipotumia risasi kuwatawanya waandamanaji katikakati mwa mji mkuu Khartoum.

Sudan imekuwa ikiongozwa na baraza la kijeshi tangu kung'olewa madarakani kwa kiongozi wa muda mrefu Omar al-Bashir aliyepinduliwa mwezi uliopita, lakini limeshindwa kurejesha taifa hilo katika hali ya utulivu.

Waandamanaji walioshinikiza kuanguka kwa utawala wa Bashir wameendelea kufanya maandamano ya kukaa nje ya makao makuu ya jeshi mjini Khartoum kudai jeshi likabidhi mamlaka kwa raia.

Ghasia za hivi karibuni zimetia dosari katika mazungumzo ambayo yalionekana kuleta matumaini ya kuundwa baraza la mpito la pamoja kati ya jeshi na raia kuongoza nchi hiyo kwa miaka mitatu hadi uchaguzi.

Advertisement