Mbaroni kwa kubaka, kulawiti watoto watano

Muktasari:

  • Yahaya Idd (58), mkazi wa Njoro manispaa ya Moshi anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kuwabaka watoto watano wanaosoma darasa la tatu Shule ya Msingi Chemchem

Moshi.  Yahaya Idd (58), mkazi wa Njoro manispaa ya Moshi anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro kwa tuhuma za kuwabaka watoto watano wanaosoma darasa la tatu Shule ya Msingi Chemchem.

Akizungumza leo Jumanne Julai 16, 2019 kamanda wa polisi mkoani humo,  Hamisi Issah amesema tukio hilo limetokea jana, kwamba wanafunzi hao wenye umri kati ya miaka nane hadi 10, wamefanyiwa ukatili huo wakati wa mapumziko shuleni.

“Watoto walitoroka na walimu aliwafuatilia ila waliporejea mmoja alikuwa akitembea kwa kuchechemea. Baada ya kuhojiwa alisema walikuwa wametoka kwa babu Yahaya ambaye amembaka mmoja wao,” amesema kamanda huyo.

Amesema uchunguzi wa awali umeonyesha watoto hao wamebakwa na mmoja kulawitiwa.

Wakizungumza na Mwananchi watoto hao wamesema wamekuwa wakienda kwa Yahaya wakiwaongozwa na mmoja wao na hupewa Sh200 na ndizi mbivu baada ya kufanyiwa ukatili huo, kutakiwa kurejea shuleni.

Watoto hao walipohojiwa na Mwananchi, wameeleza kuwa wamekuwa wakienda kwa Yahaya wakiwa kundi, kuongozwa na mmoja wao na hupewa fedha na ndizi.

“Kwa Babu Yahaya huwa tunaenda muda wa mapumziko na tumekuwa tukipelekwa na (anamtaja jina mwenzao) , kwa kuwa  mama yake amekuwa akipewa unga wa kupikia ugali na babu.

“Tunapofika  kwa mwenzetu sisi  tunawekewa filamu (ya ngono), mwenzetu akimaliza  anachofanya  anachukuliwa mtoto mgeni na babu anaanza kufanya naye tabia mbaya,” amesema mmoja wa watoto hao.