Mbeya wafungua soko la pili la madini

Monday May 6 2019

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ( wa

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila ( wa tatu kutoka kulia) akikata utepe katika uzinduzi wa soko la madini jijini Mbeya. Picha na Yonathan Kossam. 

By Yonathan Kossam, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Mkoa wa Mbeya umefungua soko jingine la madini jijini hapa baada ya lile la kwanza kufunguliwa wilayani Chunya Mei 2, 2019.

Akizungumza katika uzinduzi wa soko hilo leo Jumatatu Mei 6, 2019 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema masoko hayo yatakuwa na tija kwa wachimbaji, wanunuzi na Serikali.

"Tumeambiwa kwamba watu wa TRA, taasisi za fedha, watu wa uthamini watakuwapo hapa lakini hata bei elekezi kwa siku hiyo itakuwa wazi," amesema.

Chalamila amesema ufunguaji masoko hayo unakusudia kupunguza au kuondoa kabisa tatizo la utoroshaji madini kwa kuunda kikosi kazi kitakachoshirikiana na mikoa jirani  kukomesha tatizo hilo.

Naye Mkurugenzi Ukaguzi na Biashara ya Madini wa Tume ya Madini,  Dk Venance Mwasse amesema soko hilo ni la 13 kufunguliwa nchini na katika utekelezaji wa sheria inayoratibu masoko hayo Mbeya imefaulu kwa asilimia 100.

Naye Mwenyekiti wa Wachimbaji Wadogo Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha amesema wao kama wachimbaji wanatakiwa kutumia rasilimali ya madini kulinufaisha taifa badala ya kuonekana kuwa watoroshaji wa madini.

"Tunaomba kweli hili soko liwe kwa ajili yetu wachimbaji wadogo, lakini tunaomba idadi ya watendaji katika vituo iongezwe," amesema.

Advertisement