Mbeya watekeleza agizo mifuko ya plastiki

Saturday June 1 2019

By Yonathan Kossam, Mwananchi [email protected]

Mbeya. Leo ikiwa ndio siku ya kuanza kwa utekelezaji wa zuio la Serikali dhidi ya matumizi ya mifuko ya plastiki, wananchi na wafanyabiashara jijini Mbeya wameanza kutekeleza agizo hilo.

Mwananchi Digital leo Jumamosi Juni mosi imeshuhudia baadhi ya wananchi wakiwa wamebeba bidhaa mbalimbali kwa kutumia mifuko mbadala ikiwamo bahasha na vikapu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital baadhi ya wafanyabiashara kutoka Soko la Matola jijini hapa wamesema mteja akienda kununua bidhaa anapaswa kuwa na mfuko au chombo cha kubebea bidhaa hiyo.

Glory Kamendu ambaye ni mfanyabiashara wa ndizi amesema hakuna namna zaidi ya wateja kuja na vitu vya kubebea au atumie fedha zao kununua mfuko.

"Mteja anatakiwa aje na kitu cha kubebea kwa sababu mifuko ni gharama tofauti na ile ya awali, unanunua mifuko kwa Sh1,000 ndani inakuwa 40 tofauti na sasa mmoja unauzwa Sh500," amesema.

Naye Michael Nsemwa ambaye ni muuzaji wa bucha amesema mteja anatakiwa kuwa na chombo cha kubebea bidhaa hiyo, wao wanachoweza kutoa ni karatasi gumu kabla ya kuweka kwenye chombo cha mteja.

Advertisement

Advertisement