Mbinu hizi kuivusha Simba

Tuesday January 15 2019

 

By Charles Abel,Mwanachi [email protected]

Dar es Salaam. Simba inapaswa kufanya mambo manne makubwa ili kuvuna pointi tatu dhidi ya AS Vita ya DR Congo, katika mchezo unaofuata wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaochezwa Kinshasa, Jumamosi wiki hii.

Simba inatakiwa kuimarisha nidhamu, mbinu, kucheza kwa utulivu na umakini katika dakika zote 90 za mchezo ili kuvuna pointi tatu ugenini.

AS Vita inayoshika nafasi ya tatu kwenye Kundi D baada ya kupoteza mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Al Ahly, ni moja ya timu tishio katika mashindano ya kimataifa hasa inapokuwa uwanja wa nyumbani kutokana na ubora wa kikosi chake na mbinu inazotumia.

Kila mchezaji wa Simba atakayepata nafasi ya kucheza mchezo huo, anapaswa kuhakikisha hafanyi utovu wa nidhamu hasa uchezaji wa rafu ambazo zinaweza kuwapa wapinzani faulo zinazoweza kutumiwa na AS Vita kufunga mabao.

Timu hiyo ni hatari katika kutumia mipira ya faulo hasa ile ya jirani na eneo la hatari la wapinzani wao na imekuwa ikitumia mwanya huo kupata ushindi.

Mara kwa mara mipira hiyo ya adhabu ndogo ambayo AS Vita huipata nje kidogo ya lango la adui, inapigwa moja kwa moja na mshambuliaji Jean Mundele ambaye ni fundi wa upigaji wa faulo za aina hiyo.

AS Vita ina wachezaji wenye kiwango bora cha kufunga mabao ya vichwa kutokana na mipira ya krosi au kona lakini pia imekuwa ikitumia mbinu mbadala ya kufunga mabao kutokana na mashuti nje ya eneo la hatari.

Timu hiyo inayonolewa na kocha wa timu ya Taifa ya DR Congo, Florent Ibenge ni moja ya timu zinazojua kutumia vyema makosa ya timu pinzani kupata mabao.

AS Vita iliyocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana, ina nyota wenye ujanja wa kuwapa presha wachezaji wa timu pinzani hasa wale wanaocheza safu ya ulinzi na mbinu hii imekuwa ikiwapa faida endapo adui atafanya makosa.

Hapana shaka Mundele anapaswa kuchungwa na Simba katika mchezo huo kutokana na uwezo wake wa kufunga na jinsi anavyoweza kuwahadaa mabeki wa timu pinzani.

Mundele ukiachana na uwezo wake wa kupiga faulo, ana kasi, chenga na uwezo mzuri wa kumiliki mpira na kupiga pasi za mwisho.

Msimu uliopita, mshambuliaji huyo alifunga mabao 15 katika mashindano ya Afrika, manne alifunga kwenye Ligi ya Mabingwa huku 11 akifunga kwenye Kombe la Shirikisho.

Simba inapaswa kucheza kwa umakini hasa kipindi cha pili ambacho AS Vita imekuwa ikitumia vyema kufunga mabao yao pindi inapokuwa nyumbani.

Katika mechi 10 za mwisho za kimataifa ambazo AS Vita ilicheza nyumbani, imefunga mabao 38 ambapo 11 ilipata kipindi cha kwanza na 17 ilifunga kipindi cha pili. Katika mechi hizo 10 imeshinda mara tisa na imetoka sare katika mchezo mmoja tu.

Wasikie Pawasa, Pazi

Beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema ni lazima timu hiyo ijipange kikamilifu kabla ya kukabiliana na AS Vita.

“Kwa jinsi nilivyoitazama AS Vita, jambo kubwa ambalo Simba inapaswa kufanya ni kuandaa mpango bora wa mbinu ambayo timu inatakiwa kuingia nayo katika mchezo. Kama tutashambulia basi tushambulie na kama tutaamua kujilinda basi tunapaswa kuwa makini,” alisema Pawasa.

Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Idd Pazi alisema Simba inatakiwa kwenda DR Congo kwa tahadhari kubwa na amewataka mabeki kuwa makini.

“Bila shaka kocha ameiangalia AS Vita namna ilivyocheza na Al Ahyly, Wacongo wakicheza nyumbani ni wabishi. Simba inapaswa kuwa makini hasa mabeki ili kupunguza makosa ambayo yanaweza kuigharimu timu,” alisema Pazi.

“Waende na mbinu ya kushambulia na siyo kujilinda ili wapate sare kwani njia bora ya kujilinda ni kushambulia, lakini pia beki wa Simba, Juuko Murshid. Kama alipewa kadi ya njano dhidi ya Saoura anatakiwa kuwa makini katika mechi zinazofuata ajitahidi kuwa na nidhamu ya ukabaji,”alisema Mayay.

Nahodha huyo wa zamani wa Yanga, alisema AS Vita inapocheza nyumbani inakuwa na nguvu kubwa na morali ya mashabiki, hivyo Simba inapaswa kuwa makini.


Advertisement