Mbolea tani 97,000 zahitajika Mbeya

Muktasari:

  • Licha ya kuongoza katika uzalishaji wa baadhi ya mazao ya biashara mkoa wa Mbeya bado unakabiliwa na upungufu wa pembejeo, viuatilifu, madawa, zana bora za kilimo pamoja na masoko ya uhakika

Dar es Salaam. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema licha ya kuwa mkoa wa Mbeya unaongoza katika uzalishaji wa baadhi ya mazao ya biashara lakini bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kilimo ikiwemo uhitaji wa tani 97,862 za mbolea katika msimu ujao wa kilimo.

Ameyasema hayo leo Aprili 26, 2019 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda, Nzovwe jijini Mbeya.

Hasunga amesema miongoni mwa mazao ambayo mkoa wa Mbeya unafanya vizuri katika uzalishaji ni pareto kwa asilimia 81, kakao asilimia 53 na unachangia asilimia 16 ya tumbaku yote inayozalishwa nchini.

“Changamoto hizi za pembejeo, viuatilifu madawa na zana bora za kilimo pamoja na upatikanaji wa soko la mazao. Uliagiza tuzifanyie kazi na wewe mwenyewe umekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha masoko yanapatikana na sisi tunafanya hivyo,” amesema Hasunga.

“Tunawaomba wananchi waendelee kulima sana kwa sababu soko la uhakika lipo hasa la mahindi katika nchi za jirani,” amesema.

Akizungumzia suala la usajili wa wakulima wa mazao, Hasunga alisema mpaka sasa asilimia 76 ya wakulima wa mazao nane ya biashara wamesajiliwa huku wakulima wa pamba wakiongoza.

“Mpaka sasa wakulima wa pamba waliosajiliwa ni 600,010 huku usajili wa wananchi wanaolima mazao mengine ukiendelea hadi tutakapomaliza,” amesema Hasunga.