Mbowe, vigogo 13 kupishana Kisutu leo

Wednesday January 2 2019

 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na vigogo wengine 13 leo Alhamisi Januari 3, 2019 watafika katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusikiliza kesi zinazowakabili.

Miongoni mwa kesi hizo ni za kufanya mikusanyiko isivyo halali inayowakabili viongozi tisa wa Chadema.

Kati ya vigogo hao wa Chadema, Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko ndio wapo gerezani tangu Novemba 23, 2018 baada ya kufutiwa dhamana na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai namba 112 ya 2018 ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Katibu wa Chadema, Dk Vincent  Mashinji na mbunge wa Bunda, Ester Bulaya.

Wengine ni naibu katibu mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na mbunge wa Kawe, Halima Mdee.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 13, ikiwemo kula njama,  kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari Mosi na 16, 2018.

Kesho pia itasikilizwa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Harbinder  Seth na mfanyabiashara James Rugemalira.

Wawili hao wanaendelea kusota rumande kwa takribani mwaka mmoja na miezi saba sasa kutokana na upelelezi wa shauri hilo kutokamilika.

Wanakabiliwa na mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi ikiwemo kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu , kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi.

Pia, mahakama hiyo kesho itasikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili viongozi watatu wa klabu wa Simba.

Washtakiwa hao ni aliyekuwa rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, makamu wake, Geofrey Nyange maarufu Kaburu na mwenyekiti wa kamati ya usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Mahakama hiyo pia itasikiliza kesi ya mauaji ya aliyekuwa mjumbe wa tume ya mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya mauaji namba 6/2018 ni Msigwa Matonya (35), Mianda Mlewa(45), Paulo Mdonondo (35), Longishu Losindo (34), Juma Kangungu (34) na John Mayunga (60).

Kesho pia upande wa mashtaka na ule wa utetezi katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa watatu, akiwemo raia wa China, Yang Feng Glan (66) utawasilisha majumuisho ya mwisho ya hoja za pande zote baada ya kufunga ushahidi.

Mbali na Glan, maarufu kama malkia wa meno ya tembo, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Salvius Matembo na Philemon Manase  ambao wote wanatetewa na wakili Nehemia Nkoko.

Wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh13 bilioni kinyume cha sheria.

Kesi nyingine ni ile ya kughushi saini ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Januari  Makamba inayowakabili wafanyakazi sita wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Washtakiwa hao ni ofisa wa mazingira, Deusdith Katwale (38) na  mtaalam wa Tehama, Luciana Lawi (33); ofisa mazingira msaidizi,  Magori Wambura (38); katibu muhtasi, Edna Lutanjuka; msaidizi wa ofisi, Mwaruka Mwaruka (42) na ofisa mazingira, Lilian Laizer (27).

Advertisement