Mbowe alalamikia hotuba kuminywa, Ndugai amjibu

Muktasari:

Mbowe alisema Latifah Chande, mbunge wa viti maalumu kupitia chama hicho wakati akisoma hotuba ya upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alitakiwa na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kutosoma maneno yaliyoondolewa.

Dodoma. Wakati kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akisema kitendo cha baadhi ya maneno ya hotuba za kambi hiyo kuondolewa na Bunge hakikuwahi kutokea miaka ya nyuma, Spika Job Ndugai amesema atafuatilia suala hilo na atalitolea ufafanuzi.

Ndugai alisema kwa muda hakuwepo bungeni, hivyo baada ya Pasaka atalizungumzia suala hilo.

Mbowe akitoa madai yake jana alipozungumza na Mwananchi alisema, “wanadhibiti vyama vya siasa nje ya Bunge, mikutano ya vyama vya siasa imezuiwa, kuna kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari, walizuia vikao vya Bunge kuonyeshwa moja kwa moja na sasa maneno yetu katika hotuba yanaondolewa. Haya yote yanayominywa yana maana kubwa kwa nchi.”

Tangu kuanza kwa Bunge la Bajeti baadhi ya vitabu vya hotuba za wasemaji wa kambi hiyo kuhusu wizara mbalimbali karibu kila kurasa vimekuwa vikiandikwa ‘maneno haya yameondolewa kwa maelekezo ya kiti.’

Kwa mujibu wa kiti, maneno hayo yanadaiwa kuwa siyo ya kibunge, na hata wasemaji wa upinzani wanaposoma hotuba zao halisi huzuiwa na kutakiwa kusoma ambazo zimefanyiwa marekebisho na Bunge na kuondolewa baadhi ya maneno.

Wiki hii, hotuba ya upinzani kuhusu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iliondolewa kabisa katika kumbukumbu za Bunge baada ya msemaji wake, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuonekana kutokuwa tayari kuondoa maneno hayo, kutokana na kutaka kusoma ambayo haijafanyiwa marekebisho.

Mbowe alisema hotuba ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kuhusu Ofisi ya Waziri Mkuu haikusomwa kutokana na Spika kuwazuia kurejea bungeni na hata ambao hawakuwepo wakati wenzao wakitoka, walishindwa kuisoma baada ya Spika kueleza kuwa hakuwa amepewa maelezo na Mbowe.

Wabunge hao wa Chadema walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge baada ya mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema kukumbana na adhabu ya kutohudhuria mikutano mitatu ya Bunge kutokana na kukiri kuwa ‘Bunge ni dhaifu’, akiunga mkono kauli ya mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliyetoa kauli kama hiyo na kukumbana na adhabu ya kutohudhuria mikutano miwili.

Mbowe alisema Latifah Chande, mbunge wa viti maalumu kupitia chama hicho wakati akisoma hotuba ya upinzani kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) alitakiwa na mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kutosoma maneno yaliyoondolewa.

Katika maelezo yake, Mbowe alisema, “Bunge likiwa moja kwa moja wananchi wanaona kila kitu, lakini kwa sasa linatoa kitu ambacho wanataka wananchi wakisikie. Waliona Bunge live liliwapa wapinzani nguvu kubwa katika uchaguzi wa 2015, walitengeneza mkakati baada ya uchaguzi ili lisionekane moja kwa moja.”

Mbunge huyo wa Hai alisema zuio la Bunge kutoonyeshwa mubashara liliwafanya wapinzani kuhamia katika mikutano ya hadhara ambayo pia ilizuiwa na waliporejea kueleza mambo mbalimbali bungeni, pia maneno yao yanaondolewa jambo linalofanya yasiingie katika kumbukumbu za Bunge.

“Walibaini kuwa sekretarieti ya KUB (Kambi Rasmi ya Upinznia Bungeni) ndio huandaa hotuba na tafiti, na walifukuzwa wote mwaka jana mwanzoni na waliobaki ni sekretari, dereva mmoja na mkurugenzi ila watumishi (wengine) wote waliondolewa,” alisema Mbowe.

“Kwa sasa hawaruhusiwi kuingia katika maeneo ya Bunge, unaweza kuwafungua watu ila si kwa mawazo. Leo kambi ya upinzani ina watumishi ambao hawaruhusiwi hata kuingia ndani ya ukumbi wa Bunge.” Mbowe alisema kwa sasa wanaandaa hotuba zao nje ya Bunge na zinahakikiwa na kutakiwa kuziwasilisha siku moja kabla ya kusomwa. “Wanatoa baadhi ya maneno ambayo wanaona hayafai, na wanasema kiti kimeamua maneno yatolewe. Ni kawaida kukuta nusu ya hotuba imeondolewa,” alisema.

Akizungumzia hotuba ya kiongozi wa kambi hiyo alisema ndiyo hutoa dira kwa hotuba zote za upinzani, lakini ilizuiwa katika mazingira ambayo siyo ya kawaida.

“Spika alisahau kuwa kuna wabunge wengine wa upinzani walikuwa hawapo wakati wengine tukitoka bungeni na ikawa vigumu kuwazuia. Tukawaagiza wakaisome kwa niaba yetu lakini walikataliwa, huenda ilionekana inatoa mwanga katika masuala mbalimbali.”

Alipoulizwa nini kifanyike, Mbowe alisema, “ujenzi wa demokrasia ni safari ndefu, ni hapo ambapo Watanzania wataelezwa hili si tatizo la Mbowe wala Chadema, ACT wala CUF. Uongozi wa Bunge haututendei haki na hatujawahi kuona mambo haya katika mabunge yaliyopita.”