VIDEO: Mbowe aikosoa adhabu ya kamati ya Bunge dhidi ya CAG

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe akipinga adhabu iliyopendekezwa na Kamati ya Bunge ya Kinga, Haki, Maadili, Madaraka ya Bunge kuhusu shauri dhidi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad la kulidharirisha Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe amesema kumtia hatiani Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ni kuvunja Katiba


Dodoma. Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe amesema kama bunge si dhaifu waruhusu bunge live.

Akichangia taarifa ya kamati ya bunge, haki, kinga na madaraka ya bunge leo ambayo  ilimhoji Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za  Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kuhusu kauli yake ya 'udhaifu wa bunge' aliyoitoa wakati akihojiwa na idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, Mbowe ambaye ni mbunge wa Hai (Chadema) amesema hatua hiyo ni kutaka kuwaziba mdomo watu wasitoe maoni yao.

“Sisi hapa bungeni tunafanya uamuzi ambao unaathiri Watanzania, tunataka kupoka haki za msingi za watu kwa sababu sisi tuna mamlaka ya kufanya hivyo,” amesema.

Amesema Katiba inatoa haki na uhuru wa mawazo ambapo kila mtu akiwamo CAG ana uhuru wa kutoa maoni na maelezo bila kujali mipaka ya nchi.

“Kifungu kilichomtia hatiani (CAG) kinavunja Katiba ya nchi. Katika siku za usoni tunapounda kamati za maadili tuangalie kwa makini ‘composition’.  Kwa sababu ya  composition hii haiwezi kutoa justice (haki) kwa mbunge wa upinzani wala mtu aliye nje ya bunge ambao wanaonekana kuikwaza Serikali,” amesema.

Amesema kwa ushauri wake ili maadili ya bunge yasimamiwe sawasawa na kwa haki ni vyema uangaliwe utaratibu wa kufanya balance (usawa) kwa wajumbe.

Mbowe amesema kuendelea kuipeleka kamati ilivyo hivi sasa mtazamo wa umma unaona kuwa ni ya chama.

“Na uamuzi ni nje ya bunge, huko watu tunakuwa tunayotekeleza uamuzi tuliyopewa. Cacus (kamati) ya chama inafanya uamuzi kwa niaba ya bunge,” amesema.

“Wamemkaanga Profesa Assad kwa hoja ya Sh1.5 trilioni hadi Sh2.4 trilioni kwa sababu ametumia neno dhaifu,” amesema Mbowe.