Kauli tata ya Mbowe, Lissu kupoteza ubunge

Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe

Muktasari:

  • Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni nchini Tanzania, Freeman Mbowe amesema hatua ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kutangaza Tundu Lissu si mbunge wa Singida Mashariki hakitawarudisha nyuma katika harakati za kupigania demokrasia.
  • Spika Ndugai alisema Lissu amepoteza ubunge kutokana na utoro bugeni lakini kutokujaza fomu za mali na madeni za maadili ya viongozi wa umma

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Freeman Mbowe amesema uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai la kutangaza nafasi kiti cha ubunge wa Singida Mashariki kilichokuwa kikikaliwa na Tundu Lissu kiko wazi halijawatikisa wala kuwakatisha tamaa bali kuzidi kuimarisha dhamira yao ya kushika dola.

Mbowe  ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni Tanzania alitoa msimamo huo wa chama leo Jumamosi Juni 29, 2019 wakati wa kikao cha ndani kilichofanyika jana Kanda ya Nyasa.

Alisema chama hicho kipo tayari hata kupoteza viti vyake vyote lakini hakitaacha kufanya kazi kwa ajili ya wananchi hivyo amewataka wanachama wa chama hicho kutokuwa na mioyo ya visasi.

“Yaani Spika leo anamfukuza ubunge Tundu Lissu anafikiri tutalia, tunamwambia mheshimiwa spika wacha Lissu chukua viti vyote hivi, nani ana shida na ubunge, tuna shida na wananchi,” alisema Mbowe

“Wanatupa sababu zaidi za kufanya kazi vitu kama hivi haviwezi kutukatisha tamaa, vinatuimarisha katika dhamira yetu, tunafanyiwa uonevu mwingi ndani ya bunge, tunafanyiwa visa vingi. Hivi visa havituvunji moyo, vinatuimarisha.”

Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema, “Hasira ya kufukuza wabunge wetu, hasira ya kutoheshimu mawazo yetu, hasira ya kuondoa michango yetu tutaimaliza kwa kupeleka wabunge wengi, kuondoa wingi wa CCM ndani ya bunge na kuiongoza serikali ya nchi hii.”

Mbowe alilalamikia pia Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge kwa kuwashughulikia wabunge wa upinzani pekee huku ikionekana kushindwa kuwagusa wabunge wa CCM.

“Uonevu huu wanaotufanyia, hatuna sababu ya kuwatukana, tunacheka lakini dhamira ndani ya mioyo yetu inaimarishwa sana kila mbunge wetu angesimama kueleza anafanyiwa nini sijui ingekuwaje,” alisema