Mbowe na Zitto wahoji maafikiano DPP, washtakiwa

Wafanyakazi wa kampuni ya Vodacom wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam walikokuwa wanakabiliwa na makosa ya uhujumu uchumi. Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Kwa upande wake Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kwa sasa inaonekana kama kesi za utakatishaji fedha ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali.

Dodoma. Zitto Kabwe na Freeman Mbowe juzi jioni walizungumzia kesi za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi zilizoipatia Serikali mabilioni ya fedha.

Zitto, kiongozi wa ACT Wazalendo, alihoji sababu za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kukubaliana na baadhi ya washtakiwa na kukubaliana malipo ya mabilioni, Mbowe (mwenyekiti wa Chadema) akisema kesi hizo zimegeuzwa mkakati mpya wa kukusanya mapato.

Hoja zao zimekuja siku chache baada ya kampuni ya Vodacom kutoa taarifa kuwa imefikia makubaliano na DPP ambayo yanahusisha malipo ya Sh5.2 bilioni ili kumaliza kesi ya uhujumu uchumi dhidi ya wafanyakazi watano waliokuwa mahabusu.

Siku hiyo, mkurugenzi wa mtendaji wa Vodacom, Hisham Hendi na wafanyakazi wengine wanne walikiri makosa na suala lao kuisha.

Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Tamisemi na Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Umma na Utawala Bora), Zitto alisema DPP hukubaliana na baadhi ya washtakiwa ambao ama hulipa faini, kupunguziwa adhabu au kufutiwa mashtaka.

Alihoji DPP anafanya hivyo kwa sheria ipi na fedha hizo zinakwenda wapi.

“Tumepewa revenue books (vitabu vya mapato), kuna kila senti ambayo kila idara ya Serikali inaingiza. Nimeangalia ofisi ya DPP kwa miaka mitatu yote ya nyuma na hata mwaka huu wanatarajia kuingiza Sh14milioni tu, ila mwaka jana wamekusanya Sh23bilioni kwa watu wanaokamatwa na kumalizana na DPP na kesi zinafutwa,” alisema Zitto.

“Naomba kufahamu kwa sheria ipi, fedha zinakwenda wapi na nani anazikagua hizo fedha?

“Kumekuwa na utamaduni ofisi ya mwendesha mashtaka kukamata watu, hatujui kama wanabambikiwa kesi au la, lakini baadaye tunaona watu wale wanakubaliana na ofisi ya DPP na kulipa pesa na kesi hiyo inakwisha.

“Ningependa nchi yetu ipate ufafanuzi huenda kuna uonevu mkubwa sana. Kwamba watu wanabambikiwa kesi kwa utakatishaji fedha, wanawekwa ndani ili wazungumze na DPP halafu waende mahakamani wakiri na kulipa faini kiwango ambacho wameshtakiwa.”

Kwa upande wake Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kwa sasa inaonekana kama kesi za utakatishaji fedha ni mkakati mpya wa kukuza mapato ya Serikali.

“Imekuwa utamaduni wa Serikali kugeuza kesi za utakatishaji fedha kama chanzo cha mapato,” alisema Mbowe.

“Watu wanakamatwa, uchunguzi unaendelea miezi sita au mwaka mzima na (huku) magereza Dar es Salaam zimejaa mahabusu zaidi ya 5,000.

“Wanawarundika watu ambao walipaswa kuwa nje kwa misingi ya dhamana.”

Wakati suala la Vodacom linaweza kuwa limewasukuma wanasiasa hao wa upinzani, kesi za namna hiyo zimeiwezesha Serikali kupata takriban Sh9.23 bilioni kwa mujibu wa taarifa ambazo Mwananchi imekusanya.

Hata hivyo, hakukuwepo na maelezo kuwa kuisha kwa kesi hizo kulitokana na makubaliano kati ya washtakiwa na DPP, kama ilivyokuwa kwa Vodacom.

Kampuni za simu za Zantel na Halotel zilipigwa faini ya jumla ya Sh1.33 bilioni.

Juni 21, 2018, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliwahukumu wakurugenzi watendaji wa kampuni za Zantel na Halotel kulipa faini ya Sh238 milioni, au kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana na hatia ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh1.1 bilioni na kukiri makosa hayo.

Mbali na adhabu hiyo ya faini, pia waliamriwa kulipa fidia ya hasara hiyo waliyosaibabisha na hivyo Serikali kujipatia jumla ya Sh1.33 bilioni

Kesi nyingine ilimhusu mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam, Shabani Hussein, maarufu kwa jina la Ndama Mtoto wa Ng’ombe, ambaye alilipa Sh200 milioni baada ya kukiri kosa la utakatishaji fedha Sh540 milioni.

Katika kesi ya Vodacom, mahakama iliwaamuru washtakiwa kulipa jumla ya Sh6.01 bilioni, ikiwa ni fidia ya hasara waliyoisababisha yaani (Sh5.89 bilioni) pamoja na faini ya jumla ya Sh120 milioni.

Katika kesi ya utoroshaji wa madini ya dhahabu mjini Mwanza Hakimu Mkazi wa Mkoa, iliwahukumu kulipa faini ya jumla ya Sh529.8 milioni. Washtakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha shehena ya dhahabu kilo 323.6 zenye thamani ya Sh27.18 bilioni na fedha taslimu Sh305 milioni.

Jumla ya faini yote waliyotakiwa kulipa katika mashtaka yote waliyotiwa hatiani na mali zilizotaifishwa ilifikia ShSh834.9 milioni.

Katika ya Kesi ya Wakili Medium Mwale, iliyohusisha pia kosa la utakatishaji fedha kati ya mashtaka 44, Mahakama Kuu iliwahukumu kifungo au faini ya Sh200 milioni.

Mshtakiwa mwenzake, Donbosco Gichana (raia wa Kenya), alitakiwa kulipa faini ya Sh300 milioni, baada ya kukiri kosa la utakatishaji fedha.

DPP pia alifanikisha kupatikana kwa Sh259.5 milioni kutoka kwa mfanyabiashara wa Dar es Salaam, Akram Aziz aliyekiri mashtaka 73 ya kukutwa na nyara za Serikali ikiwemo kukutwa na nyama ya nyati na silaha.

Katika kesi nyingine dhidi ya Wathailand walioingiza nchini Sh100 milioni bila maelezo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi iliwahukumu kulipa faini ya Sh100 milioni.

Mitandaoni

Hoja ya zito iliibua mjadala na mwanasheria Alberto Msonda pamoja mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Dk Mwigulu Nchemba, walimjibu.

Katika ukurasa wake wa Twitter, Dk Mwigulu aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani alisema, “DPP haingii makubaliano na washtakiwa, wala hakamati watuhumiwa.”

“Yeye anashughulika na mashtaka baada tuhuma kujulikana na baadaye kuonekana kuna makosa na mtu anakamatwa. Ikiwa genuine case mtu hupelekwa mahakamani, akiri makosa mahakamani, anahukumiwa na mahakama sio kwa DPP.”

Naye Albert Msando aliandika katika ukurasa wake wa Instagram kuwa si kweli kwamba kuna watuhumiwa wanalazimishwa kukiri makosa na DPP.

“Sio sahihi kupotosha suala la kisheria na kuichafua ofisi ya DPP kwa sababu za kisiasa” ameandika Msando.

Habari za ziada na James Magai