Mbowe naye amtuma Lowassa CCM

Mwenyekiti wa Chadema,Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Picha na Said Khamis

Muktasari:

  • Katika mkutano huo alizungumzia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na misukosuko iliyomfanya akae mahabusu kwa kipindi kirefu na matukio ya hivi karibuni ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli aliwahi kumpa ujumbe Edward Lowassa aupeleke kwa viongozi wa upinzani, na jana ilikuwa zamu ya mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kumtuma waziri huyo mkuu wa zamani CCM.

Rais Magufuli alimsifu Lowassa kuwa ana siasa za kistaarabu wakati huo akiwa Chadema na kumtaka kuwaeleza viongozi wenzake wa upinzani watulie “la sivyo wataishia gerezani”, akisema vyama visiwe “chachu ya kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo.”

Ilikuwa Novemba 27, mwaka jana wakati wa uzinduzi wa maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako Lowassa alihudhuria.

Zikiwa zimepita siku 108 tangu Rais Magufuli atoe salamu hizo, jana ilikuwa zamu ya Mbowe kutumia njia kama hiyo baada ya Lowassaa kurejea CCM, Machi Mosi.

“Tulimpokea (Lowassa) kwa nia njema, lakini kaenda chama kingine cha siasa. Huko basi akaseme kweli na atusaidie kukieleza chama chake kipya kisiendelee kuwatesa Watanzania,” alisema Mbowe katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, jana.

Katika mkutano huo alizungumzia mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na misukosuko iliyomfanya akae mahabusu kwa kipindi kirefu na matukio ya hivi karibuni ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.

Mbowe alisema alisikitishwa kusikia Lowassa ameondoka Chadema wakati akiwa gerezani ambako pamoja na mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko wamekaa tangu Novemba 23, mwaka jana baada ya kufutiwa dhamana katika kesi yao ya jinai.

Alitoka kwa dhamana Machi 7 baada ya kushinda rufaa Mahakama Kuu.

“Mwalimu (Julius) Nyerere alizungumza wakati wa uhai wake kuwa chama cha siasa ni dodoki. Ukiliweka kwenye maji litanyonya maji, ukiliweka kwenye maziwa litanyonya maziwa,” alisema Mbowe.

“Sisi ni chama cha siasa tunawajibika kukijenga chama na kuongeza wanachama. Katika mkakati huo tulimwongeza Lowassa mwaka 2015. Vyama vyetu vinavuta watu wa makundi mengi kwa sababu mbalimbali.”

Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni (KUB) alisema wapo watu wema, wasio wema, wapenda madaraka, wanaotumwa kuwatumikia watu, lakini akasema kila mmoja ana uelewa wake na anatambua anataka nini.

“Kwa hiyo, nilisikitika. Nikisema nilifurahi nitasingizia kwa sababu tulimpokea kwa nia njema, lakini kaenda chama kingine cha siasa. Huko basi akaseme kweli na atusaidie kukieleza chama chake kipya kisiendelee kuwatesa Watanzania,” alisema Mbowe.

“Sisi tutaendelea kupigania demokrasia. Yeye na wenzake tunawatakia safari njema.”

Yaliyowapata gerezani

Wakigusia masaibu ya gerezani, Mbowe na Matiko wameilaumu Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP) kuwa inachangia ongezeko la mahabusu magerezani.

Hata hivyo, DPP Biswalo Mganga aliwataka wanasiasa hao kutoingiza siasa kwenye masuala ya kisheria.

Huku akitoa mfano wa kesi inayowakabili kina Mbowe kuwa wao ndiyo wamesababisha ichelewe kusikilizwa.

“Unajua kesi yao tulianza kuipeleka Machi mwaka jana. Tukasema tuko tayari leteni tuanze, wakaanza kuzungusha kila ikiitishwa linakuja hili,” alisema.

“Usikilizaji wa awali uliaanza Machi hadi wanafutiwa dhamana. Siku wanafutiwa dhamana ndiyo tunaanza usikilizaji wa awali, sasa anayechelewesha kesi ni nani?”

Kuhusu kesi nyingine, Mganga alisema “kesi ziko High Court (Mahakama Kuu) zinasubiri kusikilizwa na nyingine zinachelewa kwa sababu ya mashahidi”.

Hata hivyo Mbowe na Matiko walisema kucheleweshwa kwa kesi nyingi kunaumiza mahabusu wengi.

Mbowe alimuomba Jaji Mkuu, Mkuu wa Jeshi la Polisi na Kamishna wa Magereza kufanya operesheni maalumu itakayosaidia kupunguza nusu ya mahabusu waliofurika magerezani.

Akizungumzia magereza, Mbowe alisema yanakabiliwa na mlundikano na uchafu uliokithiri.

Msemaji wa Jeshi la Magereza, Amina Kavirondo alikiri kuwepo kwa idadi kubwa ya mahabusu magerezani, akisema hilo ni suala mtambuka.

“Ili mahabusu awepo gerezani kuna vyombo vya jinai vitakavyohusika. Kuna Polisi watakaokamata, kuna waendesha mashtaka, kuna mahakama kuna Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali,” alisema.

“Vyombo vyote hivyo vinaweza kujibu kwa nini kuna mlundikano wa mahabusu magerezani.

“Kwa mfano hapa Dar es Salaam kuna magereza mangapi ya mahabusu? Ni Segerea na Keko, Jiji la Dar es Salaam lina mahakama ngapi, lina wilaya ngapi na lina wahalifu kiasi gani? Katika kuwahifadhi hao, jiulize gereza la Segerea limejengwa mwaka gani. Jiulize gereza la Keko limejengwa mwaka gani kuna maajabu gani yatakayotokea?”