Mbu wabadili tabia za kung’ata, wapo waenezao dengue

Muktasari:

Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndungulile amesema kuna mabadiliko ya tabia za mbu kung’ata binadamu, wakiwemo wanaoeneza ugonjwa wa dengue


Dar es Salaam.  Naibu Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk Faustine Ndungulile amesema kuna mabadiliko ya tabia za mbu kung’ata binadamu, wakiwemo wanaoeneza ugonjwa wa dengue.

Amesema waliokuwa wanang’ata usiku au jioni kwa sasa wanang’ata mchana na asubuhi,  waliokuwa wanapiga kelele zaidi wakipita sikioni kwa sasa hawafanyi hivyo na wale waliokuwa wakiruka juu kuzidi usawa wa gari dogo kwa sasa wanaruka chini zaidi.

Ametoa kauli hiyo jana Jumanne Julai 9, 2019 baada ya kutembelea taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara hiyo  katika maonyesho ya kimataifa ya biashara yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.

“Kuna mbu wa aina tatu, Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa wanaosababisha ugonjwa wa dengue, Anopheles waoambukiza  Malaria  na Culex wanaoambukiza matende na mabusha,” amesema.

Amesema taasisi zinazofanya utafiti zinapaswa kuongeza bidii kwenye eneo hilo ili yanapotokea mabadiliko iwe rahisi kuyadhibiti.

 “Tumeweka msisitizo kwenye neti na kunyunyizia dawa ndani ya nyumba, inawezekana tunafanya hatua zote hizi lakini mbu wanakaa nje.  Tunahisi mbu wanakaa ndani kumbe wapo nje kwa hiyo chandalua inakuwa haina tija kama  mbu anauma mchana,” amesema Dk Ndungulile.

Amesema inahitajika utafiti zaidi kujua tabia za mbu ili iwe rahisi kujua namna ya kuwadhibiti.

“Taasisi  zifanye tafiti kuangalia tabia za mbu na dawa zinazotumika sasa hivi zina tija, je mbu hawa hawana usugu wa hizi dawa,” amehoji.

Akizungumzia ugonjwa wa dengue bila kutaja takwimu,  Ndugulile amesema maambukizi yameendelea kushuka na kuwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo.