Mbunge: Serikali haikufanya utafiti vitambulisho vya machinga

Muktasari:

  • Amesema wanawake na vijana wanaobeba machungwa na kuuza mchicha mtaani wanafanya hivyo kujikimu kimaisha lakini wanabanwa wakitakiwa kuwa na vitambulisho

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Tendega amehoji kama Serikali ya Tanzania ilifanya utafiti kabla ya kuanza kutoa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo maarufu machinga.

Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili 8, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu 2019/20 ikiwa ni siku moja tangu Rais John Magufuli kusisitiza suala la ugawaji vitambulisho kwa machinga kuwa litaondoka na kiongozi yeyote wakiwamo wakuu wa wilaya na mikoa watakaobainika kushindwa kutekeleza mpango huo.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana akizungumza na wananchi wa Mbinga mkoani Ruvuma muda mfupi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Mbinga hadi Mbambabay yenye urefu wa kilomita 67 itakayogharimu Sh134.712 bilioni.

Kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi ni ya pili ndani ya siku saba baada ya Aprili mosi 2019 kusisitiza kuhusu jambo hilo.

“Hivi mlifanya utafiti kwamba wajasiriamali shida yao ni vitambulisho? Maana wanawake na vijana wanabeba ungo na kuweka maembe na mchicha, hivi anatakiwa awe na kitambulisho,” amesema Tendega na kuongeza:

“Mliahidi Sh50 milioni kila kijiji leo mnakuja  na vitambulisho. Hawa watu wanakimbia maana wanauza bidhaa hizi kwa ajili ya kujikimu na kusomesha watoto nyinyi mnakwenda kuwadai.

“Mlifanya utafiti katika hili na je ndio mlilenga kuwakomboa wananchi wanyonge?  Tunapaswa tufikiri zaidi ili kuona ni mambo gani muhimu tufanye kwa maslahi ya nchi.”

Mbunge huyo alifananisha kubanwa kwa wafanyabiashara na udumavu: “Tanzania ni nchi ya tatu Afrika inayoongoza kwa udumavu na ya 10 duniani kwa udumavu wa kimwili na kiakili. Zaidi ya asilimia 42 ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano wana udumavu wa kiakili.”

“Nazungumzia hili kwa sababu tunataka tujenge taifa ambalo tutaendeleza kizazi na kizazi. Tunayoyatenga hapa katika bajeti yetu yafanye kazi ya kuendeleza vizazi na vizazi na si miaka mitano mitano.”