Mbunge Bwege amuomba Magufuli kuzungumzia kutekwa kwa watu nchini Tanzania

Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara 'bwege' akimtaka Rais John Magufuli kutoa kauli kuhusu matukio ya utekaji yanayoendelea nchini, alipokuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya maji kwa mwaka wa fedha 2019/2020 bungeni jijini Dodoma

Muktasari:

  • Sakata la mwanachama wa Chadema Mdude Nyagali kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana limeendelea kuzungumziwa bungeni huku Mbunge wa Kilwa Kisuni (CUF), Selamani Bungara akimuomba Rais John Magufuli kuzungumzia suala ya watu kutekwa

Dodoma.  Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege amemuomba Rais John Magufuli kuzungumzia masuala ya watu wanaotekwa.

Bungara ameyasema hayo leo Jumatatu Mei 6, 2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2019/20.

“Kila kizuri kinakuwa na kibaya kidogo. Namuomba Magufuli hawa watu wanaotekwa tekwa atoe kauli aseme kidogo, kina Mdude hawa nao kukaa kwake kimya...” amesema Bwege lakini kabla ya kumalizia sentensi yake Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alimkatisha na kumtaka kurudi katika hoja.

“Na muda wako huo, unga mkono jitihada za Rais Magufuli upate maji,” amesema Chenge lakini Bungara akasema anaunga mkono hoja ya upinzani.

Sakata hilo limeanza kuzungumziwa tangu asubuhi baada ya Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kuomba kutoa hoja ya dharura akitaka Bunge lijadili suala la kudaiwa kutekwa kwa mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali.