Mbunge CCM amtaka Waziri wa Viwanda kuirejesha Kariakoo ya zamani

Muktasari:

Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kueleza mikakati anayoifanya kuhakikisha Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam linarejea katika hali yake ya zamani

Dodoma. Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda kueleza mikakati anayoifanya kuhakikisha Soko la Kimataifa la Kariakoo jijini Dar es Salaam linarejea katika hali yake ya zamani.

Mtulia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 15 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara ya viwanda na biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh100.38 bilioni.

Mbunge huyo amemtaka Kakunda kukaa na wafanyakazi wa wizara hiyo ili wamsaidie akisema wana mawazo mazuri.

“Dar es Salaam ilikuwa kitovu cha biashara ila kwa sasa Kariakoo yetu iko wapi? Tunataka waziri uirejeshe Kariakoo yetu, iko wapi Kariakoo yetu ya Wanyarwanda, Warundi, Wakongo kuja kununua bidhaa.”

“Kariakoo ilikuwa Dubai yetu, mimi namtaka waziri (Kakunda) asituulize tufanye nini, biashara hazifanyiki ni aibu mfanyabiashara anakwenda kufuata mzigo Uganda, kwa nini eti kodi ni kubwa,” amesema.

Mbunge wa Mpendae (CCM), Salim Turky amesema: “Mimi ni mfanyabiashara na mwenye viwanda na hata jimboni kwangu watu walinipa kura nyingi sana kwa sababu walijua nitakuja kuwatetea.”

“Watu wanadumaza viwanda vyetu, kuna mafuta ya kampuni tatu yamekaa bandarini zaidi ya miezi saba kwa sababu ya mgongano kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao walipoyapima wakadai hayafai kwa matumizi.”

Mbunge huyo amesema wafanyabiashara hao walipoona hivyo wakapeleka malalamiko kwa waziri mkuu ambaye aliagiza  yapelekwe kwa mkemia mkuu wa Serikali kuyachunguza na yalipopimwa yakabainika kuwa ni mafuta ghafi.

“Baada ya TRA kuelezwa ni mafuta ghafi wameanda kudai document original (nyaraka halisi) hizo nyaraka halisi hatuwezi kuzipata sisi tunapata copy, hili waziri lishughulikie,” amesema.

Amesema mpaka sasa viwanda vitano vimefungwa na zaidi ya ajira 200 zimepotea huku akidai wafanyabiashara wanapitia mazingira magumu yanayohitaji kurekebishwa.