Mbunge CCM aonyesha udhaifu wa risiti za EFDs

Mbunge wa Buyungu, Christopher Chiza akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Buyungu (CCM) Christopher Chiza ameitaka Serikali ya Tanzania kufanyia ukaguzi mashine za kielektroniki (EFDs) ili kuwawezesha wafanyabiashara kupata risiti ambazo hazifutiki baada ya muda.

Dodoma. Mbunge wa Buyungu (CCM) Christopher Chiza amesema risiti za kielektroniki (EFDs) hasa zinazotolewa kwenye vituo vya mafuta hufutika baada ya muda na hivyo kuwafanya wafanyabiashara washindwe kutunza kumbukumbu.

Chiza alikuwa akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Juni 18, 2019.

Amesema Serikali inapendekeza kupunguza ushuru wa mashine za EFDs kutoka asilimia 10 hadi asilimia sifuri akisema ni jambo jema kwa sababu mashine hizo zinatumika katika kukusanya ushuru.

Amesema alihudhuria mkutano wa Chama cha wafanyabiashara, wenye viwanda na kilimo, (TCCIA)  kwa ajili kufundisha jinsi mashine za EFDs zinavyoagizwa.

Amesema walisema mashine hizo kama ilivyo kwa bidhaa nyingine wanaweza kucheza nazo hivyo wakati mwingine mashine hizo zinaweza zikawa hazitoi taarifa sahihi.

“Zikawa ama zinaiumiza Serikali ama wafanyabiashara ushauri wangu ni kuwa mashine hizo ziwe zinakaguliwa mara kwa mara. Tena aliyetuambia ni Mtu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania),”amesema.

Amesema anaamini TRA hao wanasimamia mashine hizo na hivyo jambo alilokuwa akilisema bila shaka ana imani nalo.

Amesema kwa mfanyabiashara anahitaji kutunza risiti zake ili kutunza kumbukumbu zake kwa ajili ya kukaguliwa.

“Mashine nyingi hasa kwenye vituo vya mafuta  ukiiweka nyumbani baada ya miezi mitatu minne hazisomeki tena yamefutika yote kama hujapiga picha basi hizo taarifa na kumbukumbu utakuwa hauna tena,” amesema.

Ameomba ziangaliwe na kama mashine ziboreshwe ili kuwawezesha wafanyabiashara waweze kutunza kumbukumbu zao kwa sababu ya marejeo.