VIDEO: Mbunge CCM ataka kilimo cha bangi kuruhusiwa Tanzania

Muktasari:

  • Mbunge wa Kahama Mjini (CCM),   Jumanne Kishimba ameishauri Serikali ya Tanzania kuruhusu kilimo cha  bangi nchini kwa ajili ya utengenezaji wa dawa za binadamu

Dodoma.  Mbunge wa Kahama Mjini (CCM),   Jumanne Kishimba ameishauri Serikali ya Tanzania kuruhusu kilimo cha  bangi nchini kwa ajili ya utengenezaji wa dawa za binadamu.

Amesema hayo leo Jumatatu Mei 20,  2019 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo mwaka 2019/2020.

Amesema nchi nne barani Afrika zimeruhusu kilimo cha bangi kwa ajili ya matumizi ya dawa za binadamu.

“Ni vizuri kama Dunia inapopata kitu kizuri ni vyema  Watanzania tukawahi. Ninavyoongea gazeti la Mwananchi la tarehe 15 limesema Uganda  imesharuhusu kulima bangi kwa ajili ya dawa za binadamu,” amesema mbunge huyo.

Amebainisha dawa nyingi za maumivu ya saratani asilimia 80 zinatokana na bangi, “Nashangaa wataalam wetu wa Mamlaka ya Chakula la Dawa (TFDA) wangekuwa wameshachukua sampuli na wangewajulisha kuwa dawa zilizo na bangi ndani yake.”

“Wangemuuliza  msambazaji hiyo bangi anaitoa wapi? Spika sisi wenyewe tunayo bangi hiyo tunaona kila siku inakatwa ukweli nyingi sio kwa ajili ya kuvuta. Bangi hiyo imekuwa ikienda katika dawa za binadamu.”

Amesema ana ushahidi Lesotho na Zimbabwe kuruhusu ulimaji wa bangi na kuna viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu kwa kutumia bangi.

Amesema gunia  moja la bangi nchini ni kati ya Sh4milioni hadi Sh4.5milioni na kwamba Lesotho na Zimbabwe gunia moja ni Sh20milioni.

“Bangi yote ya Tanzania inakwenda katika dawa za binadamu ambazo tunaletewa kutumia. Kuna ubaya gani ikaanza kutoa vibali kwenye maeneo mbalimbali na kuhalalisha watu waanze kulima bangi hiyo na kupata faida.” amesema.

Amesema haungi mkono kauli ya mbunge wa Geita (CCM),  Joseph Msukuma ambaye amekuwa akitaka bangi kuhalalishwa kwa ajili ya kuvuta.

 “Ni vizuri waziri wa Kilimo awasiliane na Waziri wa Afya waone namna gani watafanya. Lakini kwanza bangi ni zao ambalo haliliwi na wadudu. Eka moja ya bangi unapata gunia sita,” amesema.