Mbunge CCM ataka mawaziri waachie ngazi

Mbunge wa Busega (CCM), Raphael Chegeni akihoji kufugwa kwa biashara nyingi nchini kutokana na kutokuwepo kwa mazingira rafiki ya kwa wafanyabiashara, wakati akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya viwanda na biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020, bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Waziri wa Viwanda na Biashara ametakiwa kuachia ngazi kwa kuwa ameshindwa kumsaidia Rais John Magufuli na kufanya biashara za Tanzania kuendelea kudorora.

Dodoma.Mbunge wa Busega (CCM) Dk Rafael Chegeni amewataka mawaziri wa viwanda na biashara kuachia ngazi kwani wameshindwa kumsaidia Rais John Magufuli ambaye anahangaika na wafanyabiashara peke yake.

Akichangia leo Jumanne Mei 14, 2019 katika hotuba ya Waziri wa Viwanda, Dk Chegeni amesema hakuna kitu kinachofanywa na waziri wa viwanda na mawaziri wengine kwa kuwa wameshindwa kuwa kitu kimoja ili kuwasaidia wafanyabiashara.

Chegeni amesema mazingira ya uwekezaji Tanzania si mazuri na kuwa yanawavunja moyo wawekezaji.

Amesema watu wengi wamevunjika moyo na kukata tamaa katika mambo ya kibiashara kutokana na mazingira yaliyopo ambayo kwa sehemu kubwa hayana urafiki na wafanyabiashara.

“Mazingira hayaridhishi kabisa, kwa mfano tulimsikia naibu waziri wa fedha akisema kuwa biashara zinafungwa na nyingine zinafunguliwa, hii si kweli hata kidogo hakuna biashara zinazofunguliwa, hali ni mbaya lazima tuelezane ukweli,” amesema Chegeni.

Amesema kazi kubwa iliyobaki kwa viongozi ni kulalamika akahoji wanaolalamika wanamlalamikia nani wakati wanapaswa kutoa majibu.

“Nasema kama mmeshindwa achieni ngazi maana mtakuwa mmeshindwa kumshauri na kumsaidia Rais ambaye anafanya kazi kubwa na nzuri, hata anawaambia wafanyabiashara wakiwa na shida wamtafute, hivi kweli wamtafute Rais wote watamuona, ninyi mnafanya nini,” amehoji.

Akizungumzia suala la utalii amesema wageni wengi wanaofika nchini hukatishwa tamaa kutokana na nyuso za watumishi wa viwanja vya ndege wanapofika kwani wafanyakazi huwa wamekunja nyuso kama watu waliokula pilipili.