Mbunge CCM awaeleza wabunge wao ni maiti watarajiwa

Muktasari:

Mbunge wa Kahama Mjini (CCM) Jumanne Kishimba amechangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2019/2020 na kupendekeza kufutwa kwa tozo za maiti, wagonjwa waruhusiwe kutibiwa wakiwa na mifugo na wagonjwa kununua mashine zao za vipimo.

Dodoma. Mbunge wa Kahama Mjini (CCM) Jumanne Kishimba ameitaka Serikali kuruhusu watu wanaokosa fedha za kulipia gharama za kutunza miili ama za matibabu kwenda kuwaombea na kufahamu mahali walipozikwa ili ndugu watakapopata fedha wachukue mifupa na kwenda kuzika wanapopataka.

Kishimba aliyasema hayo juzi usiku Juni 18 2019 wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Alianza kwa kuishukuru Serikali kwa kusambaza dawa nyingi hospitali lakini akasema katika afya bado kuna matatizo.

“Sisi tunatoka mikoa ya kanda ya ziwa ambapo wenyeji wa pale ama wanakataa kukata bima kwa sababu ya tradition (utamaduni) yao kwamba wanajitabiria kifo ama kujitabiria ugonjwa,” alisema.

Aliomba wizara ya afya kuwaruhusu wanakijiji wanapokuwa ameugua kama wana kuku ama mahindi watoe katika zahanati ili baadaye zipigwe mnada.

“Kwanini nasema hivi mtu ameugua mchana ama usiku anatakiwa kwenda hospitali  na fedha hana. Na leo kuuza mfugo kazi, lakini kama atapokelewa mfugo ama mahindi atapata matibabu na vitu hivyo vitauzwa. Hakuna daktari ambaye hajui kuku wala nini,” alisema.

Alisema sasa hivi kumezuka tabia katika hospitali za Serikali na za taasisi za dini ambayo ni kutoa gharama (bill) za matibabu ya marehemu na kama huna fedha hukataa kukabidhi mwili.

“Maiti ile wanaenda kuzika kama wanatupa mbwa. Ni kitu kibaya sana. Na humu ndani nashangaa mheshimiwa Waziri Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango) sisi sote ni maiti watarajiwa kasoro itakuwa muda, tarehe na wakati,” alisema.

Alisema katika bajeti hiyo wamesamehe unga wa keki lakini wanatoza tozo la maiti na kumuomba Waziri Mpango kurejesha kodi hiyo na kufuta tozo ya maiti.

“Asilimia 95 ya vifo vinatokana na kuumwa na kuumwa kwenyewe na kuumwa kwenyewe mara nyingine ni kwa muda mrefu, kunapokuwa kwa muda mrefu huyu mtu anakuwa amedhoofika kiuchumi, amedhoofika kiafya. Sasa leo anafariki hospitali inampa bill ya Sh500,000, anazipata wapi na huyu mtu alishakufa? Aliehoji.

Alisema Watanzania wote wanalipa kodi kupitia bidhaa wanazozinunua, “Ni hatari sana nafikiri vijana wetu watengeneza bajeti ni wa Oysterbay walijua kusamehe unga wa keki ni kitu muhimu sana. Ndio maana wakashindwa kuelewa kuna shida nyingi sana kule kwetu kijijini.”

“Mheshimiwa Naibu Spika umepita kule Kahama zile nyumba unazoziona za nyasi njiani ni za waganga wa kienyeji. Waganga wa kienyeji ukipeleka mgonjwa akifariki bahati mbaya hawaombi pesa, badala yake wanakusaidia na sanda.”

Alihoji inawezekanaje Serikali kumdai maiti, kukatalia maiti na kwenda kuuizika kwa kutupa kwa gharama.

“Bahati nzuri Mheshimiwa Msigwa (Peter Msigwa-Mbunge wa Iringa Mjini-Chadema) Lwakatare (Getrude Lwakatare-Viti Maalum-CCM)  ni wachungaji wangetusaidia, turuhusiwe tukafanye maombi kule kwenye makaburi ya Serikali na wajue makaburi ya ndugu zao ili baadaye watoto wakipata fedha wakachukue mifupa ya baba yao,” alisema.

Alisema katika bajeti hiyo wamefuta kodi katika unga wa ngano ambao unatengeneza vyakula na kuhoji vyakula gani kama sio keki na biskuti.

Aidha, alisema mashine za X Ray na kusafisha figo zinauzwa kati ya Sh40 milioni hadi  Sh100 milioni na kuhoji kwa nini huduma hizo hutolewa kwa Sh200,000 hadi Sh40,000.

“Kwanini Serikali isiruhusu watu wanunue mashine wazipeleke hospitali ili bei ya (huduma) X ray ipungue. Najua wataalam wataleta maneno mengi ambayo yanahusu afya lakini ni uongo mhehimiwa Naibu Spika,” amesema.

Alisema ni uongo kwa sababu waganga wa kienyeji wanapewa kibali na Wizara ya Afya kuendesha shughuli zao na hawana elimu yoyote.

“Kule kwetu mheshimiwa Naibu Spika mgonjwa mahututi ndio anapelekwa kwa mganga wa kienyeji ambako hakuna choo hakuna chochote. Ni vipi leo Serikali wakatae watu wanunue wapeke hizo X Ray ili bei hii ipungue?” alihoji.