Mbunge CUF adai aliahidiwa Sh200milioni ahamie CCM, Polepole amjibu

Muktasari:

Hadi leo Februari 14, 2019 wabunge wa upinzani waliohamia CCM ni, Maulid Mtulia, Dk Godwin Mollel, Mwita Waitara, Julius Kalanga, Zubery Kuchauka, Ryoba Chacha, Joseph Mkundi, James Ole Millya, Pauline Gekul, na Abdallah Mtolea.

 


Unguja. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya CUF (Juvicuf), Hamidu Bobali amesema viongozi wa CCM waliwahi kumuahidi kumpatia Sh200milioni sambamba na kuteuliwa kuwa naibu Waziri endapo angekubali kujiunga na chama hicho tawala.

Bobali ambaye pia ni mbunge wa Mchinga kwa tiketi ya chama hicho ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 14, 2019  katika mkutano wa jumuiya hiyo.

Amesema ujasiri ulimfanya ashinde majaribu hayo, akibainisha kuwa mbali na mamilioni hayo, pia aliahidiwa kuwa atateuliwa kuwa naibu waziri.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, mbunge huyo amesema kilichomfanya ashindwe kujiunga na CCM ni utu na uzalendo huku akiwashangaa wabunge wa upinzani waliohamia CCM kwa maelezo kuwa wamewasaliti wananchi waliowachagua.

Awali, Maalim Seif aliwataka vijana wa chama hicho kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanailinda CUF na kutokubali kurubuniwa.

Alipoulizwa kuhusu madai ya mbunge huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole  amesema chama tawala hakijawahi kuahidi kumpa mtu yeyote fedha ili ajiunge nacho.

Amebainisha kuwa wabunge na madiwani wote wa vyama vya upinzani  waliohamia CCM walikwenda kwa hiari yao kutokana na kasi ya  maendeleo inayofanya na Rais John Magufuli.

“Madai ya Bobali hayana ukweli na hayapaswi kujadiliwa na wala wananchi wasipoteze muda kuhusu kauli zake,” amesema Polepole.