Mbunge CUF amtuhumu wa CCM kwa ‘utekaji’

Mbunge wa Kilwa Kusini, Selemani Bungara akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadiro ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Wakati Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara akidai jana Jumatano Aprili 24 bungeni jijini Dodoma kuwa mbunge mwenzake wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka gari yake imehusika katika tukio la utekaji, amejibiwa na mbunge huyo kuwa ni mzushi

Dodoma. Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Seleman Bungara ‘Bwege’ amemtuhumu mbunge mwenzake wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka kuwa gari lake lilihusika katika tukio la utekaji mkoani Lindi.

Bwege ametoa tuhuma hiyo jana jioni Jumatano Aprili 24 bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ya mwaka wa fedha 2019/2020, huku Kuchauka akijibu mapigo kuwa madai hayo si ya kweli.

Bwege amedai katika uchaguzi mdogo wa Kilwa Kivinje watu watatu walitekwa na kwamba kati ya magari yaliyohusika na utekaji huo ni la Kuchauka huku akitaja namba za gari hilo.

“Lugola (Kangi-Waziri wa Mambo ya Ndani) ulinishauri nifungue kesi cha kusikitisha waliofanya utekaji wanajulikana na magari waliyotumia yanajulikana likiwamo la Kuchauka lakini hadi leo hawajakamatwa,” amesema Bwege.

Baada ya kauli hiyo, Kuchauka aliomba taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge na kukanusha madai hayo.

“Asipotoshe Bunge maana hiki ni chombo maalum, gari yangu mimi haikuwa na namba anazozitaja,” amesema Kuchauka na kutaja namba halisi za gari yake.

Akijibu taarifa hiyo Bungara amesema: “Mimi taarifa nimetoa polisi na hiyo gari haikukamatwa kwa sababu wanamlinda. Sasa kama si kweli kwanini asikamatwe na hiyo namba anayosema ilivyoingizwa katika kumbukumbu ilionekana ni Scania siyo  Toyota Landcruiser. Lile ni gari yako na ushahidi upo.”

Bwege alimuomba Lugola kufuatilia jambo hilo huku akisema Tanzania ni nchi huru, hawajawahi kushuhudia matukio ya namna hiyo.

“Mwaka jana hapa bungeni nilisema kuna vijana wangu watatu wamekamatwa mpaka leo hatujui walipo, nakuomba waziri Lugola fuatilia hili maana wakati ule nilimueleza aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani, Mwigulu Nchemba lakini hakunijibu kitu,” amesema.

Kuhusu kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara na maandamano mbunge huyo amesema ni kinyume na katiba ya nchi.

“Mbaya zaidi hata pale Rais Magufuli (John) aliporuhusu wabunge tufanye mikutano katika majimbo yetu bado polisi wanatuzuia. Binafsi nimezuiwa na polisi kufanya mikutano mitano, juzi tu hapa nilizuiwa eti kwa sababu Mpina (Luhaga-Waziri wa Mifugo na Uvuvi) amechoma nyavu za wavuvi nikifanya mkutano hali ya hewa itakuwa mbaya,” amesema..

Bwege amedai Aprili 20 mwaka huu, Rashid Salio Rashid alikamatwa na kupelekwa mkoani Mtwara na kwamba hadi sasa hajulikani alipo.